Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kupitia Upya Mashamba Yaliyofutwa na Rais Magufuli Kilosa
May 17, 2019
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema wizara yake itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Raisi katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.

Lukuvi amesema hayo leo katika Kata ya Chanzulu, Tarafa ya Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro alipozungumza na wananchi wa kata hiyo wakati alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Waziri Lukuvi alisema, katika maeneo mbalimbali yapo mashamba yaliyofutwa na Rais Dkt. Magufuli lakini hayajawekewa utaratibu wa kuyatumia na hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawiya na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais Dkt. Magufuli katika Wilaya ya Kilosa na kuzuia mgogoro baina ya wananchi na wamiliki wizara yake imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki mashamba yote yaliyofutwa katika Wilaya ya Kilosa.

Kwa mujibu wa Lukuvi timu hiyo inajumuisha Kamishna wa ardhi nchini, Mary Makondo, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Samweli Katambi, Mthamini Mkuu wa Serikali Evalyne Mugasha, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitlya na Wataalamu kutoka idara za Mipango Miji Wizarani.

Alisema, uamuzi wa kwenda na timu kutoka Wizarani unalenga kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo hasa baada ya kubaini ofisi za wilaya na mkoa wa Morogoro kushindwa kutatua mgogoro huku viongozi wake wakituhumiwa.

Waziri Lukuvi alitaja kazi kubwa itakayofanya timu hiyo kuwa ni kupitia mashamba 15 yaliyofutwa na Rais Dkt. Magufuli sambamba na kufufua mipaka ya mashamba hayo na kazi hiyo itafanywa kwa na ushirikiano wa ngazi za wilaya.

"tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na Rais Dkt. Magufuli na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa" alisema Lukuvi

Huku akishangiliwa na wananchi wa Chanzulu Lukuvi alisema, wale wote waliojimilikisha mashamba yaliyofutwa na  Rais Magufuli watanyang'anywa na kupatiwa wanaostahili na mengine yatatolewa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya kupatiwa wawekezaji.

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira katika Halmashauri ya Kilosa, Ibrahim Mndembo alisema, jumla ya mashamba 25 yenye ukubwa wa hekari 23,596 kwenye maeneo ya Msowero, Magole na Chanzulu katika Wilaya ya Kilosa yamebatilishwa umiliki baada ya wamiliki wake kushindwa kuyaendeleza ambapo kati ya mashamba hayo mashamba 15 yalibatilishwa miliki zake katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

Mashamba yenye mgogoro na wananchi katika wilaya ya Kilosa ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza dhidi ya wananchi wa Mabane, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai dhidi ya wananchi wa Ilonga na shamba la Mauzi Estate Malangali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi