Na Mwandishi Wetu, OWMS, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuanza kupanga mikakati ya kuendeleza Sekta ya Sheria nchini kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
Hayo yameelezwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akitoa salamu kwenye kikao kazi cha Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Sheria wa kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na Halmashauri zote nchini.
Dkt. Luhende ameongeza kuwa, kikao kazi hicho kimewakusanya viongozi hao ili kupanga mikakati ya kuendeleza Sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu ili kupata wanasheria wabobezi ndani ya Serikali ili kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake ambapo maelezo hayo yamejikita kwenye Kauli Mbiu ya Mwaka huu isemayo, “Utekelezaji wa Majukumu Unaozingatia Sheria ni Nyenzo Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa.”
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ambaye ndiye muandaaji wa kikao kazi hicho alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kuelewa dira na dhima ya Ofisi wanazotumikia kufanya tathmini na kujipima namna wanavyotekeleza majukumu, kufanya uchambuzi wa wadau wa ndani na nje ya taasisi wanayofanyia kazi, kuweka mikakati endelevu ya kujengeana uwezo, kuepuka kujenga uadui na makundi, kufurahia kukoselewa na kufanyia kazi maeneo waliyokosolewa na kuwa waadilifu ili wawe na nguvu ya kuchukua hatua.
“Utumishi wa umma tunaoutaka kwenye Sekta ya Sheria ni kuhakikisha kuwa kila Mtumishi wa Umma wa kada ya sheria atumike kutokana na uwezo wake mahali alipo ambapo anaweza kuwa mwajiriwa wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lakini akatumika kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa siku hizi tunasoma kuwa mahiri na sio kusoma bora tu kusoma na mpaka sasa tuna jumla ya Mawakili wa Serikali 2,661 ambapo kati ya hao Mawakili 18 wana shahada ya uzamivu, 789 wana shahada ya uzamili, 863 wana astashahada ya juu na 855 wana shahada ya kwanza ya masuala ya sheria kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Mfumo wa Taarifa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (OAG-MIS) ambapo Mawakili hao wamejisajiri,” amesema Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi waliotoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambao wameshiriki kikao kazi hicho, Shaban Ramadhan Abdallah, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa wamekuja kujifunza ili nao waweze kuiga na Kwenda kutekeleza mashirikiano hayo baina ya Ofisi hiyo ya SMZ na za Tanzania Bara
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Slyvester Mwakitalu amesema kuwa baada ya kikao kazi hicho na Mkutano wa Mawakili wa Serikali utakaofanyika tarehe 29 na 30 Septemba, 2022 utawawezesha viongozi na washiriki kupata maarifa mapya pamoja na uzoefu kwa kuwa taasisi moja inafanya mambo yanayotekelezwa na taasisi nyingine kwa kuwa taasisi za Serikali zinafanya kazi kwa kutegemeana