Na Daudi Manongi.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imelenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka katika maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba leo, Mjini Dodoma, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame Duniani inayofanyika tarehe 17 Juni kila mwaka.
“Ukataji wa miti kiholela na uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi mkubwa wa binadamu wa kupata mahitaji kutokana na mazao ya misitu pamoja na huduma zingine muhimu, kunazidisha ukubwa wa tatizo hili,” alisema Mhe.Makamba.
Aidha, Mhe. Makamba amesema kutokana na athari hizo Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti wa mwaka 2016-2021 ambao unalenga kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na kuhakikisha kwamba kila mwananchi anahusika katika utaratibu huo.
Amesema kuwa, mkakati huo pia umetoa maelekezo juu ya programu za upandaji miti, kuandaa mpango bora wa matumizi ya ardhi, kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa, ufugaji bora na wa kisasa na kusisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa pamoja na kuhifadhi maji katika kipindi cha mvua.
Mhe. Makamba ametoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu, ambayo ni “Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa manufaa ya baadaye” ili kuhakikisha ardhi ya Tanzania inatunzwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe 17 mwezi juni ya kila mwaka kuwa ya maadhimisho ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.