Serikali imesema itaendelea kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ili wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya Hifadhi wanufaike na maeneo hayo kwa kuendesha shughuli za utalii badala ya kulima mazao yanayopendwa na wanyamapori hao.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka wakati wa kikao cha nne cha Kamati Tendaji ya Usimamizi wa Mradi wa Kuzuia na Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya nyara.
Prof. Sedoyeka amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti katika kuhakikisha kuwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori inadhibitiwa kabla ya kuleta madhara ili wananchi waweze kufurahia uwepo wa wanyamapori.
" Tunataka kuona migongano baina ya binadamu na wanyamapori inapungua ili wananchi wazidi kutoa ushirikiano katika kuimarisha ulinzi wa wanyamapori wakubwa wakiwemo tembo na faru ambao wapo hatarini kutoweka" Amesema Prof. Sedoyeka.
Amesema wananchi wakinufaika na shughuli za uhifadhi watakuwa mstari wa mbele katika kuwafichua majangili kabla hawajawadhuru wanyamapori, hivyo Wizara inafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha wanyamapori wakali na waharibifu hawaathiri maisha ya wananchi.
Prof. Sedoyeka amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kutoa mafunzo kwa wanavijiji, kununua vitendea kazi yakiwemo magari pamoja na kujenga vituo vya askari kwa ajili ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapokaribia makazi ya wananchi.
Katika hatua nyingine , Prof. Sedoyeka ametoa onyo kwa wananchi waache kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima katika mapito ya wanyamapori ili kuepuka kupata hasara.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kikao cha nne cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuzuia na Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya nyara , Christine Musisi amesema suala la kupunguza migongano kati ya Binadamu na Wanyamapori linahitaji ushirikiano baina ya Serikali na wananchi wanaoishi katika maeneo karibu na Hifadhi.
"Mojawapo ya kipaumbele katika mradi wetu ni kuhakikisha tunatoa mafunzo kwa jamii jinsi ya kujikwamua kiuchumi ikiwemo ufugaji wa nyuki pamoja na kutoa mafunzo kwa wanakijiji namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu", amesema Musisi.
Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Christine Musisi amesema mradi huo utaendelea kuzinufaisha jamii kufanya shunguli zingine za kiuchumi na kuachana na vitendo vya ujangili kwa kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwakwamua kutoka kwenye umaskini