Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaongeza magari mengine 28 kwa ajili ya Ofisi za Mikoa za Idara ya Kazi na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
“Serikali itaendelea kuziwezesha idara na taasisi zake kutekeleza majukumu yao kwa kuwajengea mazingira bora ya kazi ikiwemo upatikanaji wa vitendea kazi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, inao mpango wa kuongeza magari mengine 28 ambapo kati ya hayo, magari 8 ni kwa ajili ya Idara ya kazi na 20 kwa ajili ya OSHA,” amesema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 7, 2023) wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria hafla ya kugawa vitendea kazi na magari 30 ambapo 17 ni ya ofisi za mikoa za Idara ya Kazi na 13 ni ya OSHA. Hafla hiyo ilifanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu zilizoko Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema magari hayo 30 yamenunuliwa kwa fedha za ndani na ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa katika maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi, 2023 mkoani Morogoro. “Lengo kuu ni kuimarisha taasisi na idara mbalimbali za Serikali ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi, wafanyakazi, waajiri na wawekezaji kwa ujumla,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma wafanye kazi kwa bidii na wawatumikie wananchi kwa na kusuluhisha kero zao ikiwa ni njia ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Mkaongeze bidii ya kufanya kazi na kuzingatia maadili katika utumishi wa umma ili kuonesha kwa vitendo shukrani zetu kwa Mheshimiwa Rais.”
Akisisitiza juu ya utunzaji wa magari hayo, Waziri Mkuu amesema: “Kila idara iliyopokea magari inao wajibu wa kusimamia matumizi na kuyatunza ili yadumu. Magari ya Serikali yatumike kwa shughuli za umma tu badala ya shughuli binafsi; watendaji wakuu hakikisheni magari haya wanapewa madereva wenye sifa na kusisitizwa kuyahudumia vizuri ili yadumu.”
“Tumieni magari hayo kuwafikia wananchi, hakuna sababu ya kutofanya kaguzi na kutatua kero za wananchi. Upande wa OSHA, idadi ya kaguzi iongezeke, mmepewa vitendea kazi muhimu vya kutekeleza majukumu yenu. Upande wa Idara za kazi, idadi ya mashauri mnayotatua iongezeke na kuhakikisha mnatembelea maeneo ya kazi ikiwemo migodi ili kutatua malalamiko ya wafanyakazi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watenge muda wa kwenda kusikiliza kero za wananchi katika maeneo yao badala ya kukaa ofisini muda wote. Pia alisisitiza kwamba wananchi wanaofika ofisini kwao wasikilizwe na kuhudumiwa kwa wakati na kuwapa majibu ili wasipoteze muda mwingi kufuatilia majibu ya hoja zao.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako alisema Idara ya Kazi ilikwama kiutendaji kwa sababu ilikuwa na magari manane tu kwenye mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza, Tanga, Arusha, Pwani, Mtwara na Morogoro.
Alisema magari hayo na vifaa vya kupima afya na usalama mahali pa kazi vina thamani ya sh. bilioni 4.3 na vimetolewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi hao.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamuhokya alisema anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutekeleza maombi yao kwa haraka.
“Wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2023 tuliiomba Serikali ikumbuke taasisi zake za mikoani. Tulimuomba Mheshimiwa Rais kwa sababu tunaona hali halisi huku mikoani. Hatukutegemea kama utekelezaji ungekuwa wa haraka hivi, tunamshukuru sana. Tunatumaini hayo magari yataongeza ajira kwa madereva 30.”
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE), Meneja wa Kanda ya Kati Dodoma, Bw. Selestine Leonard aliwataka waajiri na wafanyakazi waendelee kuzingatia usalama wa mahali pa kazi.
“Niwasihi waendelee kuzingatia uadilifu na hasa kujali muda wa kazi. Pia wajiepushe na vitendo vya rushwa mahali pa kazi. Sisi ATE tutaendelea kushirikiana nao,” alisisitiza.