[caption id="attachment_42990" align="aligncenter" width="750"] Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adeladius Kilangi (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), leo Jumatatu 13 Mei 2019, kuhusu uwasilishwaji wa notisi ya Rufaa ya Kesi ya kikatiba ya kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Katikati ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Clement Mashamba na kulia ni Naibu Wakili Mkuu Wa Serikali, Dkt. Ali Posi.
Na Mwandishi Wetu
Serikali imewasilisha notisi Mahakama ya Rufaa kupinga sehemu ya uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Bob Chacha Wangwe dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Taifa Uchaguzi kuhusu Wasimamizi wa Uchaguzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Mei 13, 2019, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, amesema kuwa pamoja na kuwa Ofisi yake haijapokea nakala ya hukumu lakini tayari imewasilisha Mahakama ya Rufaa kupinga baadhi ya vifungu vilivyobatilishwa na Mahakama Kuu.
“Leo tarehe 13 Mei, 2019, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewasilisha Mahakama Kuu ya Rufaa Tanzania notisi ya kukata rufaa kupinga sehemu ya uamuzi wa uliotolewa na Mahakama Kuu. Aidha, pamoja na notisi hiyo, Serikali imeomba kupatiwa nakala ya uamuzi na mwenendo wa Shauri hili”, ameeleza Profesa Kilagi.
Amesema kuwa maamuzi ambayo Serikali imeyakatia rufaa kuwa ni pamoja na Mahakama Kuu kubatilisha vifungu 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi vinavyowataka Wakurugenzi wa Majiji, Halmashauri, Miji, Wakurugenzi wa Wilaya na Wateuliwa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoka katika utumishi wa umma kusimamia uchaguzi kwa madai kuwa vinakinzana na Ibara ya 74(14) ya Katiba inayozuia anayehusika na uchaguzi kujiunga na Chama chochote cha siasa.
Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa mlalamikaji, Bob Wangwe alitaka mahakama ivibatilishwe Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachomtambua Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye anateuliwa na Rais ambapo mlalamikaji alitaka kifungu hicho kibatilishwe kwa madai kuwa kinakinzana na Ibara ya 21(1), 21(2) na 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema Serikali inapinga hoja hizo kwani Wakurugenzi ambao mlalamikaji anataka wanyang’anywe jukumu la kusimamia uchaguzi, hutekeleza jukumuhilokwa kubanwa na masharti yanayosimamia uchaguzi chi ya Sheria za Uchaguzi na kwamba huwajibika chini ya Sheria ya Sheria ya Uchaguzi na si vinginevyo.
Aidha, Katika uamuzi wa kesi hiyo, mahakama ilituppilia mbali maombi ya Bob Wangwe na kuridhia uhalali wa Kikatiba wa Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ambacho kinamtambua Mkurugenzi wa Taifa wa Uchaguzi ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia mahakama imeridhia uhalali wa Kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteua Wasimamizi wa Uchaguzi kutoka miongoni mwa watumishi wa umma.
Mei 10, 2019, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa uamuzi kuhusu Shauri la Kikatiba namba 17 la mwaka 2018 lililofunguliwa na Bob Chacha Wangwe kupinga baadhi ya vifungu vua Sheria ya Taifa ya Uchaguzi vinavyohusu Wasimamizi wa Uchaguzi kuwa vinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho. Shauri hilo lilifunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Taifa yaUchaguzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi.