Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama amewaomba wananchi kuchangamkia fursa za uchumi zitakazochochewa na ujenzi wa masoko ya mazao yanayotarajiwa kujengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Wito huo umetolewa jana wakati wa ziara yake ya kutembelea na kujionea miradi ya maendeleo katika Jimbo la Peramiho lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakati akizungumza na wananchi katika matukio tofauti katika kata mbili za Mbingamwalule na Peramiho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama katika matukio tofauti wakati akitafuta mahitaji ya nyumbani katika Soko la Peramiho “A” lililopo katika Halmashauri ya Songea.
“Tumepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya mazao, tutajenga soko kubwa Peramiho. Tutajenga Mpitimbi, Matimila, Mbingamwalule, na tutajenga soko katika Kijiji cha Muhukuru,” alisisitiza Mhe, Mhagama
Alifafanua kwamba ujenzi wa miundombinu ya barabara ya lami kuanzia Kata ya Mbingamwalule inayoenda hadi Kizuka ni ufunguzi wa uchumi kutoka Mpaka wa Tanzania na Msumbiji na utasaidia kutoa mazao shambani kwenda kwenye masoko ya mazao.
Mhe. Waziri Mhagama aliongeza kuwa, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea imepanga kuunganisha kituo cha mabasi kitakachojengwa Kata ya Mbingamwalule ili kusaidia wageni kufika kwa urahisi kwenye soko la mazao lililopo kwenye katika kata hiyo, hivyo kufungua fursa mbalimbali za uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe. Menas Komba amesema ujenzi wa soko la mazao katika Kijiji cha Matomondo kilichopo katika Kata ya Mbingamwalule, halmashauri ilipokea jumla ya shilingi milioni 198 ambayo inatekeleza mradi na ujenzi unaendelea.
“Tunataka kukamilisha ujenzi wa vyoo ili tuwalete wachuuzi waliopo mtaani kwenye soko, ili waanze kuzoea kutumia soko jipya la mazao wakati tukimalizia ujenzi kwenye baadhi ya maeneo ya soko,” alisema Mhe.Menas