Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuja na Mfumo Maalum wa Kuzuia Makundi ya Tembo Kuvamia Makazi ya Watu
Jul 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imejipanga kuja na mfumo maalum wa kuwavisha tembo kola zijulikanazo kama visukuma mawimbi ili kutambua mwelekeo wao kwa ajili ya kuwazuia kuingia katika makazi ya watu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika ziara yake ya kusikiliza changamoto za wanyama wakali na waharibifu iliyofanyika leo Kijiji cha Goha, Kwalukonge na Kweisewa, Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

 “Makundi ya tembo ambayo yanaonekana kuzagaa tutayaingiza kwenye mtambo na tembo viongozi tutawafunga kola zijulikanazo kama visukuma mawimbi na tutayafuatilia yameenda wapi.” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema kupitia njia hiyo Askari wa Uhifadhi wataweza kuwafuatilia kwa karibu na endapo kundi lolote la tembo litakuwa na mwelekeo wa kuingia kwenye makazi ya watu, watalizuia kabla ya madhara kutokea.

Aidha, ameahidi kujenga kituo cha Askari wa Uhifadhi katika vijiji hivyo ili kurahisisha zoezi la kuzuia uharibifu unaofanywa na tembo.

Pia, amesema Serikali imejipanga kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu ambapo vijana watafundishwa mbinu mbalimbali.

Kuhusu kifuta jasho/machozi ameahidi kuwa Serikali itawalipa waathirika wote ifikapo mwezi wa nane mwaka huu.

Awali, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Goha, Mohamed Ramadhani amesema kuwa tembo wamekuwa wakivamia mashamba kila ifikapo saa 4 usiku na hivyo kuiomba Serikali kuwapeleka Askari wa Uhifadhi ili kuwa kuwasaidia wananchi kukabiliana na adha hiyo.

“Inatakiwa kila Kijiji tuwe na watu wa TANAPA ili tutoke nao kukabiliana na tembo wakati wa usiku wanapokuwa mashambani na pia watupe elimu ya kukabiliana nao” amesema Bw. Ramadhani.

Naye, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mnzava ameiomba Serikali kuangalia namna bora ya kuweka uzio ili kuzuia tembo, kujenga kituo cha askari wa wanyamapori na pia kuelimisha wananchi kuhusu mbinu za kupambana na tembo wanapovamia makazi yao.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za kusikiliza changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi