Na Mwandishi wetu - ARUSHA
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema ipo bega kwa bega na Kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu cha TPI kilichopo jijini Arusha ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa ziara yake jijini Arusha leo.
"Serikali haina budi kuipa ushirikiano TPI ili kuweza kuwasaidia kuboresha utengenezaji wa dawa nchini ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 80 iliyopo na kupiga hatua zaidi" alisema Dkt. Ndugulile
Aidha Dkt. Ndugulile amewataka TPI kufuata taratibu na masharti pamoja na kukidhi vigezo vya utengenezaji wa dawa zenye viwango kwa matumizi bora ya binadamu.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TPI, Bi. Zarina Madabida amesema kuwa kiwanda kipo katika hali nzuri ya kuzalisha dawa muhimu ili kuondokana na changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.
"Tumeanza kuzalisha dawa za maji (syrup) na kuwafilka watanzania kupitia MSD ila mpaka kufikia Januari 2018 basi tunaamini tutapiga hatua zaidi ya kuwafikia watanzania wengi zaidi" alisema Bi. Madabida.
Baada ya hapo Dkt. Ndugulile alipata nafasi ya kutembelea kituo cha Afya cha Nduruma kujionea hali ya utoaji huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hiko na uboreshaji wa miundombinu katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndugulile amesema kuwa kituo kimepiga hatua utoaji wa huduma za afya kwani kina dawa zote muhimu kwa asilimia 85 na wametumia vizuri milioni 500 walizopata kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya dawa,vifaa tiba na ukarabati wa kituo chao.
"Naupongeza uongozi wa Kituo cha afya cha Nduruma kwani milioni 500 tuliyowapatia wameitumia vizuri karibia asilimia 80 ya ujenzi wa jengo la maabara, Jengo la upasuaji, Jengo la mama na mtoto, mochwari pamoja na nyumba ya watumishi vimekamilika pamoja na ununuzi wa dawa" alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile ameitaka Kamati.ya Afya ya kituo cha afya Nduruma kuhakikisha dawa zinapokelewa kwa usahihi ,matumizi sahihi ya dawa hizo na utunzaji sahihi wa dawa hizo ili kuboresha huduma ya afya kijijini hapo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile yupo kwenye ziara ya siku mbili mkoani Arusha ili kujirigdhisha na utoaji wa huduma za afya mkoani humo.