Serikali iimeendelea kutoa kipaumbele na kujizatiti katika kuimarisha ulinzi na usalama ili wananchi na wafanyabiashara waendelee kutekeleza shughuli zao za maendeleo nchini.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi.
“Serikali imejizatiti na inaendelea kutoa kipaumbelea katika kuimarisha ulinzi na usalama nchini kwa maana hii tunaendelea kuwezesha vikosi vyetu mbalimbali ili kufanya nchi yetu kuwa salama na tulivu. Ndio maana tunaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa,” amesema Rais Samia.
Ameongeza, “niwaombe sana muimarishe dhana ya ulinzi shirikishi, dhana hii ijengeke na kuimarika ili kila mmoja alipo ahakikishe kwamba usalama wa mahali alipo unamtegemea yeye”.
Kuhusu kuimarisha mazingira ya kazi na makazi ikiwa ni pamoja na kuongeza zana na vitendea kazi, kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na mafunzo kwa askari, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Tume ya Haki Jinai iliwasilisha mapendekezo yake juu ya changamoto zilizobainika kwa taasisi, ambapo kuna changamoto zinazozikabili taasisi za Haki Jinai likiwemo Jeshi la Polisi na aliahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Kamilius Wambura amesema kuwa hali ya nchi ipo salama, shwari na tulivu inayowawezesha wananchi kuendelea na majukumu yao ya kukuza uchumi wa taifa. Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha usalama barabarani na kuweka mikakati mahsusi ya kuzuia ajali za barabarani ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa wananchi.