Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuhakikisha Wanaunga Mkono Juhudi na Mikakati ya Kuwaenzi na Kuwatunza Watoto
Oct 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha zinaunga mkono juhudi na mikakati ya kuwaenzi na kuwatunza watoto zinazochukuliwa na vijiji vya kulelea watoto SOS hapa nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Rajab Yussuf Mkasaba aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya Kikanda ya Kujadili Mradi wa kuwaunganisha watoto wa vijiji vya SOS kwenye familia zao za asili yaliyofanyika huko katika hoteli ya Visitors Inn Jambiani Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini alisema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi na mikakati inayochukuliwa na Serikali zote mbili hapa nchini katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini alitumia fursa hiyo kuwaeleza washiriki hao wa mafunzo hayo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini kazi kubwa inayofanywa na kijiji cha kulelea watoto cha Zanzibar SOS na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake katika Mradi wa kuwaunganisha watoto wa vijiji vya SOS kwenye familia zao za asili.

Aliupongeza uongozi wa vijiji vya kulelea watoto SOS kwa kuichagua Zanzibar hasa Wilaya ya Kusini na kufanya mafunzo hayo ya siku tano ambayo yalijadili masuala mbalimbali juu ya mustakbali wa watoto pamoja na haki zao za msingi katika nchi zenye vijiji vya kulelea watoto SOS.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika uongozi wao wamekuwa wakifanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, hivyo kuna kila sababu ya kuungwa mkono”,alisema Mkasaba.

Aidha, Mkasaba alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa kwa nchi zenye vijiji vya kulelea watoto SOS na kuvipongeza vya kulelea watoto SOS vya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuandaa mafunzo hayo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya alizipongeza nchi za Denmark, Norway, Austria, Finland na nyenginezo kwa kuendelea kuviunga mkono na kuvisaidia vijiji vya kulelea watoto SOS katika nchi mbali mbali za bara la Afrika.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul alipongeza hatua hiyo ambayo alisema kwamba itasaidia kwa kkasi kikubwa kuwaenzi na kuwatunza watoto hapa nchini.

Nao washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi zote zenye vijiji vya kulelea watoto SOS walieleza kwamba juhudi za makusudi watazichukua katika kuhakikisha mafunzo waliyoyapata wanayafanyia kazi katika nchi zao.

Naibu Waziri huyo aliwahakikishia washiriki hao kwamba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Walieleza kwamba mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa ili watoto waweze kuishi kwa amani na upendo.

Washiriki kutoka nchi mbalimbali zenye vijiji vya kulelea watoto SOS walihudhuria mafunzo hayo wakiwemo kutoka nchi ya Denmark, Ghana, Ethiopia, Kenya, Malawi, Botswana, Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi