Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuhakikisha Mbolea Inawafika Wakulima kwa Wakati
May 04, 2018
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma.

Serikali itahakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima kwa wakati katika msimu ujao ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo hapa nchini hali itakayoongeza ari ya utekelezaji wa dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Charles Tizeba amesema kuwa katika msimu ujao, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea na pembejeo nyingine katika maeneo yao wakati wote wanapohitaji.

“Tutaandaa utaratibu maalum wa kuwajengea uwezo wabunge wote kuhusu utaratibu mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja ili Waheshimiwa Wabunge waweze kutoa maoni yao hali itakayosaidia kuboresha mfumo tuliouweka wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja”, alisisitiza Dkt. Tizeba

Akifafanua zaidi, Dkt. Tizeba amesema kuwa ni matumaini yake kuwa baada ya wabunge kujengewa uwezo watakuwa na uelewa mzuri kuhusu utaratibu huo hali itakayoondoa sintofahamu iliyopo kuhusu utaratibu mpya wa uagizaji na usambazji wa mbolea kwa pamoja.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, akijibu swali la mbunge wa Hanang Dkt. Mery Nagu aliyetaka kujua ni kwa nini vocha zimepungua na lini Serikali itaanzisha mfumo mpya wa pembejeo.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa ili kuboresha usambazaji wa pembejeo kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2017/2018 mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement system- BPS) umeongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi, bei nafuu na wakati.

Aidha, kwa kutumia utaratibu huo bei za mbolea aina ya DAP na UREA zimepungua kwa wastani wa asilimia 30.

“Serikali kupitia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja hutoa bei elekezi kwa kuzingatia umbali kutoka makao makuu ya wilaya kwenda Kata na vijiji”, alisisitiza Mhe. Dkt. Mwanjelwa.

Akifafanua zaidi, Dkt. Mwanjelwa alisema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na pindi ukiukwaji wa bei elekezi unapobainika hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika.

Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha kilimo kwa kuwekeza katika pembejeo, mbolea na zana zinazoweza kuikuza sekta ya kilimo ili iweze kuchochea uchumi wa viwanda

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi