Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kugharamia Mazishi Waliopoteza Maisha Ajali ya Ndege Bukoba: Waziri Mkuu Majaliwa
Nov 07, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Awataka Watanzania Kuwa Watulivu Waatalamu Wanapochunguza Chanzo cha AJali


Na Georgina Misama - MAELEZO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea kwa masikitiko na uzito mkubwa tukio la ajali ya ndege ya abiria Precision Air inayofanya safari zake kutoka Dar es salaam-Mwanza-Kagera iliyotokea Novemba 6, katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Amesema kufuatia ajali hiyo iliyosababisha vifo vya Watanzania 19 na majeruhi 24, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesitisha shughuli zingine ili kuungana na Watanzania kufuatilia tukio hilo kwa njia ya mtandao na kuwasilisha salamu zake za pole kwa Wanabukoba, Wanakagera na Watanzania wote kwa msiba huu.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Serikali kugharamia mazishi ya abiria wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo, hivyo nawataka Wakuu wa Mikoa katika maeneo husika kusimamia kikamilifu mazishi ya ndugu zetu waliotangulia mbele za haki,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wananchi kuwa watulivu mpaka hapo timu ya wataalam itakapokamilisha zoezi la uchunguzi  na kutoa taarifa kwa umma sambamba na kuzitaka kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi ya Mikoa  na Halmashauri kuimarishwa ili ziweze kuchukua hatua za haraka pale maafa yanapotokea katika maeneo yao.

“Nawapongeza wavuvi waliokuwepo eneo la tukio kwa kutoa msaada wa uokozi, kwa mchango wenu mliouonesha namuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Maafa kufika kuonana na kundi la wavuvi ili kuona namna wanavyoweza kuwaendeleza kwa kuwapatia mafunzo ya maafa,” alisema Waziri Mkuu.


Vilevile alisema, Rais Samia ameagiza kijana aliyeiona ndege ikitua kwenye maji na kwa ujasiri wake akaamua kwenda kufungua mlango ili kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili apatiwe nafasi katika Jeshi la Uokozi.


Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama na unazingatia viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa na kuwatoa hofu Watanzania waendelee kutumia usafiri huo kwa kuwa Mamlaka husika zipo zinasimamia na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha uwepo wa usalama wa anga kwa ajili ya safari za ndani ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi