Na Mwandishi Wetu
Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya uchunguzi kufuatia kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Baftaha Akwilini, aliyefariki kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa Serikali itahakikisha uchunguzi huo unafanyika kwa weledi na utaalamu ili haki iweze kupatikana na yeyote aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
“Nawasihi watanzania kuwa na subira ili uchunguzi ufanyike na tutahakikisha uchunguzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo na baada ya kukamilika wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria”, alisisitiza Masauni.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako alisema kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo ambacho kilitokea wakati wa kudhibiti maandamano yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la Mkwajuni, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi Akwilina na anaungana na wazazi, familia, ndugu, jamaa na watanzania wote kuwapa pole za dhati kutokana na msiba huo”, alisema Ndalichako.
Aidha Ndalichako alibainisha kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itagharamia shughuli zote za mazishi ya mwanafunzi huyo na amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia shughuli zote za msiba huo.
Pia Ndalichako alitoa rai kwa watanzania kujiepusha na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.