Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kufanya Maboresho Makubwa ya Mfumo wa Ununuzi
Oct 30, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Peter Haule na Haika Mamuya, WFM, Iringa

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, amesema kuwa Serikali imeweka udhibiti wa mianya ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma uliosababishwa na kasoro katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (TANePS) kwa kufanya maboresho makubwa ya mfumo huo.

Hayo yamebainishwa mkoani Iringa wakati alipofanya ziara ya kukagua maboresho ya mfumo huo yanayofanywa na wataalamu wa ndani kwa lengo la kuondoa changamoto zilizopo na kukidhi mahitaji halisi ya Serikali na wazabuni.

Mhe. Chande alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya kupata thamani halisi ya fedha katika huduma na bidhaa kutokana na mianya ya rushwa iliyokuwepo katika mfumo wa manunuzi ambayo inasababisha utofauti mkubwa wa gharama kwenye eneo moja.

“Kumekuwa na usiri mkubwa katika michakato ya  ununuzi, hali inayofanya mtu ajiulize huu usiri una nini katikati yake, ununuzi unatakiwa ufanyike kwa uwazi na haki, hivyo wataalamu mnaofanya maboresho haya mnaweza kututengenezea mfumo unaoakisi uhalisia katika ununuzi na utakaosaidia manunuzi kufanyika kwa haki”, alisema Mhe. Chande.  

Alisema kuwa nia ya Serikali ya kufanya maboresho hayo ni kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoka katika mazoea ya kufanya michakato ya ununuzi nje ya mfumo kwa kuwa ununuzi wa nje ya mfumo unaongeza uwezekano wa rushwa na upotevu wa thamani ya fedha.

Aidha, Mhe. Chande alisema zipo faida nyingi ambazo Serikali itazipata baada ya maboresho hayo kukamilika ikiwemo kuimarika kwa uchumi wa nchi kwa kuokoa mapato ya Serikali yanayopotea kwa kuwa asilimia 70 ya matumizi yote ya bajeti ya nchi yameelekezwa katika ununuzi.

Pia, alimtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakumu Maswi, kuhakikisha wote wanaotakiwa kutumia mfumo huo wanautumia, kwa kuwa itasikitisha kuona wataalamu wanatumia muda na nguvu zao  katika kufanya maboresho ya mfumo halafu wengine wanakaidi kuutumia.

Mhe. Chande ameipongeza PPRA kwa juhudi wanazoendelea nazo za kusimamia maboresho makubwa katika mfumo wa ununuzi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Sekta ya Ununuzi nchini

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakumu Maswi, alimuahidi Mhe. Naibu Waziri huyo kuwa maboresho ya mfumo huo yatauwezesha kuwa bora katika nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.

Pia atahakikisha wote wanaotakiwa kuutumia mfumo huo wanasajiliwa ili lengo la kufanya kazi za ununuzi wa umma kwa uwazi linafikiwa na kuwa chachu ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, aliipongeza Serikali  kwa  kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha yanafanyika maboresho makubwa ya mfumo wa ununuzi wa umma kwa kuwa  si jambo rahisi kuingia katika maboresho hayo bila kuwa na msaada kutoka  kwa wataalam wa nje ya nchi.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia mfumo huo iwapo wanataka kufanya biashara na Serikali kwa kuwa utakuwa rahisi kuutumia na umeangalia hali halisi ya mtanzania na soko la ndani.

Uamuzi wa maboresho ya Mfumo wa Ununuzi nchini ulitokana na agizo la Waziri wa Fedha  na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 bungeni. Maboresho hayo yaliyoanza mwezi Julai 2022 yanatarajiwa kufanyika kwa awamu sita ambapo mpaka sasa awamu ya kwanza tayari imekwisha kamilika na  inatarajiwa majaribio yake yaanze mwezi Desemba 2022.  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi