Na: Lilian Lundo
Serikali imesema kuwa pamoja na huduma za bidhaa ya fedha kuamuliwa na nguvu ya soko kwa upande wake imekuwa ikichua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinapungua katika soko hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Khatibu Haji juu ya Serikali inachukua hatua gani ili benki ziweze kupunguza viwango hivyo vya riba.
"Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ni pamoja na kuzitaka benki za biashara kutumia mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (Credit Reference Bureau System). Aidha, Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89," amesema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji amezitaja hatua nyingine zilizochukuliwa kuwa ni Benki Kuu kushusha riba (Discount Rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 pamoja na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirememnt (SMR)) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0.
Vile vile Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema baada ya hatua hizo za kisera kuchukuliwa na Serikali, baadhi ya benki za biashara hapa nchini zimeanza kupunguza riba za mikopo.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinaendelea kupungua.