TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo hapa nchini, kuwa katika mwaka 2018 Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, kuboresha miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga, kuongeza uzalishaji wa umeme na kukabiliana na vikwazo vya biashara.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 09 Februari, 2018 katika hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kutokana na dhamira hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi zao, kuja hapa nchini kuwekeza na kufanya biashara mbalimbali na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Aidha, Mhe. Rais magufuli amesema mwaka 2017 ulikuwa wenye mafanikio makubwa kwa Serikali kitaifa na kimataifa, ambapo iliendelea kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka 5 (2016/17-2020/2012) unaolenga kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi kulikowezesha kuongezeka kwa mapato kwa asilimia 7.87, ikiwemo rekodi ya juu kuwahi kufikiwa hapa nchini ya ukusanyaji wa Shilingi Trilioni 1.66 mwezi Desemba 2017.
Mafanikio mengine ni ukuaji mzuri wa uchumi wa asilimia 6.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017, kudhibiti mfumuko wa bei uliokuwa chini ya asilimia 5.5, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za kijamii zinazowagusa zaidi wananchi kama vile afya, elimu na maji.
Kuhusu azma ya kujenga viwanda, Mhe. Rais Magufuli amesema utekelezaji wa azma hii unakwenda vizuri ambapo katika kipindi cha miaka miwili viwanda 3,500 vimejengwa na vingine vingi vinaendelea kujengwa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kama ilivyofanya katika mwaka 2017 Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kushiriki katika juhudi za kutafuta amani, kushiriki harakati za usuluhishi wa migogoro ikiwemo ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudani kusini.
Hata hivyo ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani kwani kwa kufanya hivyo itadhohofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na nia njema ya mpango wa majaribio wa kutafuta suluhu la kudumu ya tatizo la wakimbizi (Comprehensive Refugee Response Framework – CRRF) Tanzania imeamua kujitoa kutokana na changamoto za kiusalama na ukosefu wa fedha za kugharamia mpango huo.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania zikiwa zimehusika katika uhalifu na kuwahakikishia Mabalozi hao kuwa meli hizo sio za Tanzania bali zilijipatia usajili wa Tanzania, na kwamba kufuatia hali hiyo Tanzania imechukua hatua ya kusitisha usajili wa meli zote 470 zenye usajili wa Tanzania na kusitisha zoezi la usajili mpya wa meli wakati uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika.
Kwa upande wake Naibu Kiongozi wa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa hapa nchini ambaye ni Balozi wa Saharawi Mhe. Brahim Salehe El-Mami Buseif amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na kuongeza ukusanyaji wa mapato na ameahidi kuwa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Februari, 2018