Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inaendelea na mchakato wa kufanya mapitio ya sera ya TEHAMA ya mwaka 2016, ili kuiboresha na kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Selestine Kakele, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wanawake, ikiwa ni sehemu ya maandalizi katika kuelekea kwenye Kongamano la Saba la TEHAMA 2023, litakalofanyika Oktoba 18- 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
“Sera yetu ya TEHAMA ambayo tunaipitia kwa sasa ina nguzo kuu sita ambazo ni miundombinu ya kidigitali, usimamizi wa mazingira wezeshi, elimu ya kidigitali na uendelezaji ujuzi, ubunifu, kujenga uchumi wa kidigitali jumuishi unaowafikia watu wote pamoja na huduma za kifedha za kidigitali,” amesema Bw. Kakele.
Amesema kati ya nguzo hizo sita, nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali inakusudia kupunguza na kuondoa pengo la watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali, na wasiopata fursa hiyo ambayo inaweeka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa za kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii.
Aidha amesisitiza kuwa, wajibu wa msingi wa serikali yoyote duniani ni kuweka mazingira rafiki ya kukuza na kuibua ubunifu, kuchochea uwekezaji na uendelezaji wa teknolojia za kisasa za TEHAMA ambapo zinafanya hivi kwa kutunga na kusimamia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema, mkutano huo wa siku tano utawapa fursa wadau kujadili mambo ya msingi katika sekta hiyo yakiwepo ya maendeleo na changamoto wanazokutana nazo Wanawake na Vijana katika TEHAMA nchini Tanzania.