Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuanzisha Kurugenzi ya Kusimamia Fukwe kwa Ajili ya Utalii
Oct 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inatarajia kuanzisha Kurugenzi ya kusimamia fukwe za bahari kwa ajili ya kupanua wigo wa mapato yatokanayo na sekta ya  utalii .

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Japhet Hasunga ameyasema hayo leo  wakati alipotembelea makao makuu ya Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) jijini Dar es Salaam ambapo amezungumza na watumishi wa bodi hiyo na kuwataka wawe wabunifu katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.

Amesema licha ya kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na fukwe nyingi lakini fukwe hizo zimekuwa hazitumiki ipasavyo katika kuliingizia taifa mapato kupitia utalii.

Amefafanua kuwa Kurugenzi hiyo itakayoundwa itakuwa na jukumu la kusimamia fukwe zote nchini ikiwa pamoja na  kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji ili waweze kuziboresha kwa ajili ya watalii wa ndani na nje ya nchi

Pia ametoa wito kwa Wawekezaji wenye nia ya kutaka  kuwekeza kwenye fukwe hizo ambazo zitakuwa zikisimamiwa na Kurugenzi hiyo  wakae tayari kwa ajili ya  kuchangamkia fursa hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Hasunga   amewataka watumishi hao wawe wabunifu badala ya kuendelea kulalamika kuwa  bajeti ya kujitangaza haitoshi

Hata hivyo, Naibu Waziri Hasunga amesema  anatambua kuwa bajeti wanayopewa  haitoshi katika kujitangaza lakini  ni lazima waje na njia  mbadala ya kuhakikisha kuwa bajeti hiyo hiyo ndogo inaleta matokeo makubwa.

Aidha, Amewataka wasijikite pekee katika kusafiri kwenda katika  maonesho ya  kimataifa  badala yake watumie njia nyingine za kujitangaza kwa kuanza   kuhamasisha utalii wa ndani mashuleni na vyuoni.

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, TTB itumie fursa hiyo kujitangaza kwa gharama ndogo lakini matokeo yake yawe makubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Devotha Mdachi amemueleza Naibu Waziri Hasunga kuwa licha ya ufinyu wa bajeti wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kutangaza vivutio vya utalii na watazidi kubuni njia nyingine za kutangaza kwa gharama ndogo zaidi.

Amesema kutokana na  umuhimu wa kutangaza vivutio vya utalii, TTB imeandaa Onesho la Swahili International Expo ambalo litaanza Oktoba 12 mwezi huu ambapo jumla ya Washiriki 170 kutoka nje za nchi watashiriki.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi