Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango mkubwa uliotolewa na marehemu Balozi Paul Rupia wakati wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu.
“Moja ya jambo ambalo halitasahaulika ni uthubutu wake wa kuanzisha Benki ya Watu wa Dar es Salaam (DCB) ambayo alikuwa Mwenyekiti wake na hadi anaondoka katika uongozi aliicha benki hiyo ikiwa na matawi manane na moja kati ya hayo likiwa jijini Dodoma.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema hayo leo Ijumaa (Septemba 23, 2022) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais Samia amenituma kuja kumuwakilisha katika msiba huu, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Balozi Rupia, hakuweza kuhudhuria kwa sababu yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya kikazi. Pia ametoa pole kwa familia na waombolezaji wote.”
Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Watanzania kumuombea marehemu na familia yake kwa Mwenyezi Mungu ili apate pumziko la milele na familia iwe na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema marehemu Balozi Rupia alichangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya uchumi nchini na kuanzisha mageuzi ya kisiasa ya mfumo wa vyama vingi nchini.
Awali, Mwenyekiti wa Mabalozi Wastaafu wa Tanzania, Balozi James Msekela amesema marehemu Balozi Rupia atadumu katika historia ya Tanzania kama mwanasiasa mahiri na mwanadiplomasia nguli.