Na Mbaraka Kambona, Pwani
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali imejipanga kuwawezesha Wavuvi vifaa vya kisasa ikiwemo boti kwa lengo la kuwawezesha kuvua samaki kwenye kina kirefu ili waongeza uzalishaji wa samaki, kuinua uchumi wao na kukuza Pato la Taifa.
Ndaki alibainisha hayo wakati wa hafla fupi ya kuzindua na kukabidhi jengo jipya kwa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi cha Dunda (BMU) kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa rasilimali za bahari katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi iliyofanyika wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani Julai 5, 2022.
Alisema kuwa Serikali inataka kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi na ndio maana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza bajeti ya Sekta ya Uvuvi ya Mwaka 2022/2023 ambapo sehemu yake itatumika kununua boti zaidi ya mia tatu (300) ili wakopeshwe wavuvi kwa lengo la kuboresha shughuli zao.
Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitasaidia wavuvi kwenda katika kina kirefu na kuvuna mazao mengi ya samaki na kufanya viwanda vya kuchakata samaki kufanya kazi kwa uwezo wake tofauti na ilivyo sasa ambapo viwanda vingi vinafanya kazi chini ya uwezo uliosimikwa.
Aidha, Waziri Ndaki aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupiga vita uvuvi haramu huku akisisitiza kuwa kazi hiyo siyo ya Wizara ya Mifugo na uvuvi peke yake bali ni ya kila mmoja.
"Samaki ni lishe, samaki ni pesa, samaki ni biashara na samaki ni ajira, tushirikiane kupiga vita uvuvi haramu," alisema
Halikadhalika aliwataka Viongozi wa Vikundi Shirikishi vya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi kuwa waadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa na upendeleo kwani ndio chanzo cha uvuvi haramu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainabu Abdallah aliishukuru Serikali kwa namna ilivyojipanga kuwawezesha wavuvi akiamini kuwa kwa mipango hiyo ya Serikali, Wavuvi katika Wilaya yake watanufaika kupitia shughuli zao hizo.