WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano iko imara na inamipango madhubuti ya kuwahudumia na kuwatumikia Watanzania katika maeneo yote nchini.
Ili kutimiza adhima hiyo, Waziri Mkuu amepiga marufuku kitendo cha watumishi wa umma kumaliza wiki wakiwa maofisini na badala yake amewataka watumie siku nne kwenda kwa wananchi katika maeneo yao.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Maramba wilayani ya Mkinga, Tanga.
“Ni lazima wananchi wahudumiwe wakati wote. Watumishi wa umma ni marufuku kumaliza wiki nzima mkiwa ofisi mnatakiwa kutumia siku mbili ofisini na siku nne zilizobaki nendeni mkasikilize kero za wananchi katika maeneo yao na kuzipatia ufumbuzi,”
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zote zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa. “Fedha hizi tunazoleta ni za moto zisidokolewe zitawaunguza.”
Kufuatia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya ya Mkinga, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo watenge fedha za mapato ya ndani na kuanzisha miradi ya uchimbaji wa visima wakati Serikali ikiendelea kulishughulikia suala hilo.
Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Mkinga ahakikishe wananchi wanaokwenda kufuata huduma za matibabu katika vituo vya afya na zahanati wanapatiwa dawa badala ya kuelekezwa kwenda kununua kwenye maduka.
Alisema Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 37 hadi sh bilioni 269, hivyo hakuna sababu ya mwananchi kwenda kwenda eneo la kutolea huduma ya afya na kukosa dawa. “Lazima mhakikishe dawa zote zinazotakiwa zinakuwepo kwenye zahanati na hivyo hivyo kwenye vituo vya afya na hospitali.”
Kuhusu ombi la mbunge wa Mkinga Danstan Kitandula la kutaka wananchi wapewe mashamba yasiyoendelezwa ili waweze kuyatumia katika shughuli za kilimo, Waziri Mkuu alisema atalifanyia kazi suala hilo.
Pia, Waziri Mkuu aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao na kwamba changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za upatikanaji wa huduma za maji, umeme na miundombinu ya barabara zitafanyiwa kazi.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya ya Mkinga ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda wao mwingi kutafuta maji.
Waziri Mkuu alisemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Kuhusu suala la upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu alisemamaeneo hayo yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vya wilaya hii ya Mkinga. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”
Kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alizindua miundombinu ya kituo cha afya cha Maramba ambayo ilifanyiwa ukarabati na kusema kwamba Serikali itaendelea kukiimarisha kituo hicho ili kukiboresha huduma za afya kwa wananchi.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 3, 2020.