Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewataka watumishi wanaokaribia kuhitimisha utumishi wao wa umma hivi karibuni kuhakikisha wanawekeza mahali au katika miradi ambayo ni sahihi ili iwasaidie katika maisha yao yote na ya wategemezi wao.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya wastaafu watarajiwa yanayoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yaliyofanyika jijini humo kwa siku mbili, Septemba 25 – 26, 2023.
“Niendelee kutoa wito kwa watumishi wanaotarajia kustaafu kuwekeza mahali sahihi, ndugu zangu, tafuteni fursa sahihi za uwekezaji, hasa kwa mliopo Dodoma kwani kwa sasa ni Makao Makuu ya Nchi, ni mji unaokua kwa kasi hivyo kuna fursa nyingi ambazo bado hazijatumika.Tushirikiane na Serikali kuwekeza katika huduma ambazo watu watazitaka”, amesema Mhe. Senyamule.
Amefafanua kuwa, wastaafu wengi wakistaafu wanaenda kupumzika majumbani wakati wengi wanastaafu wakiwa na nguvu, akili, ujuzi na maarifa hali ambayo sio sawa na badala yake wanatakiwa wabadilishe ujuzi na maarifa waliokuwa wanatumia kwa Mwajiri na kupeleka mahali ambapo wanafkiri wataweza kuleta tija.
“Bado mna uwezo wa kufanya kazi, mnaweza kuendelea kutumika katika sehemu mbalimbali za uzalishaji, mawazo yenu bado yanahitajika kwa faida ya mtu binafsi, watu wengine na Serikali, hivyo naendelea kuwasisitiza kuwa kustaafu ni umri tu lakini sio nguvu”, amemalizia Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi. Beatrice Lupi amesema kuwa, kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Mfuko umeandaa semina kwa wastaafu watarajiwa ili kuhakikisha maisha baada ya kustaafu yanaendelea kuwa ya staha na furaha baada ya utumishi uliotukuka ambapo hilo linawezekana tu pale wastaafu wakiwa na uhakika wa ukwasi sambamba na afya bora, vilevile wakiishi mazingira yasiyokuwa hatarishi.
“Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, takribani wastaafu 11,000 wanatarajiwa kustaafu kwa mwaka huu na katika semina za awamu hii ambazo zinahitimishwa leo, mafunzo haya yameshafanyika Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Morogoro na hapa Dodoma,” amesema Bi. Lupi.
Nae Mstaafu mtarajiwa, Mhandisi Salum Omary, amesema kuwa baada ya mafunzo waliyopatiwa, wameahidi kuwa wataweza kuwekeza sehemu salama, “hatuwezi kula mbegu kwani tukila mbegu hatutaweza kurudi shambani”, alimalizia Mhandisi Omary.