Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sekta ya Umma Kushindanishwa Tuzo za Mwaajiri Bora
Dec 20, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu  kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) imedhamiria  kuishindanisha sekta ya Umma katika tuzo za mwaka 2020 ili ushindani huo unaofanywa katika sekta binafsi uyashirikishe mashirika ya umma  kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya  kuweza kuboresha mazingira ya kazi na ajira  na kuongeza  tija hapa nchini.

Akiongea katika hafla ya tuzo ya mwaajiri bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), jijini Dar es salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, na watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, aliye mwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amefafanua kuwa ustawi wa wafanyakazi sio kwa sekta binafsi peke yake ni pamoja na sekta ya umma, hivyo ili sekta binafsi iiwe injini ya kuendesha uchumi wa Taifa,  ni lazima pia sekta ya Umma nayo iwekeze rasilimali watu ili kuweza kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

“Niipongeze ATE kwa kuwa na tuzo hizi, tungependa kuona ni mashirika gani ya Umma yanafanya vizuri katika kuangalia ustawi wa wafanyakazi na kuleta tija nchini. Maamuzi ya kuwa na washindi wa jumla  katika makundi ya kisekta yataongeza chachu mpya ya mashindano amabayo itakuza sekta mbalimbali na hatimaye yataboresha na kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu”, amesisitiza, Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama ameitaka ATE kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo ya kazi na juu ya sheria za kazi na usimamizi wa rasilimali watu ambapo kutokana na mafunzo hayo yatasaidia kupunguza migogoro mahala pa kazi na hivyo kujenga mazingira tulivu ya kibiashara ndani ya maeneo ya kazi. lakini pia mafunzo hayo huwasaidia wafanyakazi kukidhi ushindani wa mazingira ya kibiashara  kwa sasa.

“Takwimu zinaonesha mafunzo ambayo yameratibiwa na kuandaliwa na ATE kuwa vijana  1, 437, waliidhinishwa na kupata nafasi kwa waajiri huku kwenye tovuti ya serikali wapo vijana 6,919,  walijiandikisha hadi Julai mwaka huu, hivyo nitoe rai kwa waajiri wapeni fursa  vijanaili waweze kujifunza kwa vitendo,  niipongeze Kampuni ya TCC kwa kuwa mstari wa mbele kutoa nafasi kwa vijana kujifunza kwa vitendo hapa nchini.” Amesema, Mhe. Mhagama.

Aidha. Amewataka waajiri kuendelea  kushirikiana na serikali katika kutekeleza mpango wa kitaifa wa miaka 5 wa kukuza ujuzi ambao hufadhiliwa na serikali kupitia tozo ya kukuza ujuzi mahala pa kazi ili kuweza kuongeza ujuzi kwa vijana na kutatua tatizo la ajira nchini huku akiwasisitiza kuzingatia sheria za kazi zinazo onya ajira kwa watoto.

Mhe. Mhagama amewataka waajiri kuendelea kuchangia katika mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ili kuweza kuwakinga wafanyakazi dhidi ya majanga yatokanayo na kazi. Pia amewasisitiza waajiri kuzingatia haki, usawa mahala  pa kazi ili kuondoa unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi hivyo katika kuhakikisha hilo linafanikiwa serikali tayari imeshazindua mkakati wa Kitaifa wa usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe.  Stella Ikupa amewapongeza ATE kwa juhudi zao za kuunga juhudi za serikali za kuwawezesha watu wenye Ulemavu hivyo amewasihi waendelee kujenga mazingira rafiki mahala pa kazi ili watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalum waweze kufanya kazi  na kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Jayne Nyimbo amefafanua kuwa ushirikiano wanaoupata serikalini wa kushirikiana na sekta binafsi umesaidia kuboresha kwa tuzo hizo ambazo zimekuwa zikiboresha mazingira ya kazi na ajira hapa nchini.

Awali akiongea katika Hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt Aggrey Mlimuka amesema tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka mwaka huu imefanyia kazi ushauri uliotolewa na seriikali mwakk na  Waziri Mhagama kuwa katika tuzo za mwaka huu ziongeze vipengele vipya vitatu (3) ambavyo viezifanya tuzo za mwaka huu kuwa na Jumla ya vipengele 38 kutoka vipengele 35.

"Vipengele vilivyoongezeka ni Mwajiri Bora anayeendeleza Mafunzo ya Ujuzi wa Kazi kwa wahitimu (Internship), Mwajiri Bora anayetoa mafunzo ya Uanagenzi (Apprentiship), Mwajiri Bora anayezingatia Haki Rasilimali ijulikanavyo kama “Local Content”, " Alisema, Dkt.  Mlimuka.

Tangu mwaka 2015 Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kilianzisha Tuzo ya Mwajiri Bora kwa kila mwaka,   lengo la tuzo hizo ni kutathmini na kutambua  waajiri wenye mikakati bora ya usimamizi wa rasilimali watu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara na kuwahamasisha waajiri kufuata taratibu za kitaifa na kimataifa katika uendeshaji wa biashara zao ambapo makampuni wanachama kutoka sekta binafsi hushindanishwa kwa kila mwaka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi