Sekta ya Mawasiliano inachangia kukua na kuendelea kwa sekta nyingine ikiwemo kuleta ustawi wa maisha ya wananchi kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 18, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa vipaumbele vya Taasisi hiyo kwa mwaka 2023/24.
“Kutokana na mchango huo, Sekta ya Mawasiliano imekuwa ya kimkakati na ya msingi katika maendeleo ya uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu nchini Tanzania, kuanzia ngazi ya mtu binafsi, ngazi ya kaya, Taasisi na kitaifa. Utoaji wa huduma za mawasiliano ni wa ushindani hivyo umesababisha kuongezeka kwa idadi ya mitandao, matumizi ya TEHAMA na aina za huduma zinazotolewa kwa wananchi, Taasisi na Serikali kwa ujumla.”, alisema Dkt. Jabiri.
Alifafanua kuwa, kuenea kwa huduma hizo kunawezeshwa na uwepo wa sera imara, sheria nzuri na mifumo wezeshi ya kiusimamizi na utoaji leseni. Ambapo TCRA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) kwenye sekta ya mawasiliano.
Dkt. Jabiri aliongeza kuwa utekelezaji Dira hiyo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo unahusisha mchango wa TCRA kwenye uchumi kwa kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa lengo la kuboresha uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu.
Alitaja malengo mengine kuwa “Kuendelea kuweka mazingira bora ya ushindani kwenye sekta ya mawasiliano ili wananchi wengi waweze kumudu gharama za huduma za mawasiliano, kulinda watumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya uhalifu mtandaoni kwa kutumia mifumo ya kiusimamizi, kugawa rasilimali za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na masafa na kutoa leseni kwa watoa huduma zinazowezesha kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo 2025” alieleza Dkt. Jabiri.