Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sekta ya Madini Kuchangia Asilimia 10 Ifikapo 2025
Aug 18, 2023
Sekta ya Madini Kuchangia Asilimia 10 Ifikapo 2025
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024.
Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Muelekeo wa Sekta ya Madini unalenga katika kuhakikisha Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa Mwaka 2019/2020-2023/2024.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024.

“Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Tume ya Madini inatarajia kuwa na mikakati ifuatayo ili kuwa na shughuli za madini ambazo ni endelevu  za kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi yaani Halmashauri, Polisi, TARURA & TANROADS, hii  itasaidia kuuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani”, ameeleza Mhandisi Lwamo.

Mhandisi huyo ametaja baadhi ya mikakati kuwa ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususan utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia masoko na vituo vya madini nchini, kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege kwa lengo la kusaidia kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki.

Aidha, uboreshaji na usimamizi thabiti wa Mfumo wa Utoaji wa Leseni za madini utasaidia  kupunguza migogoro itokanayo na muingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji.

Pia, Mhandisi Lwamo amesema kuwa, kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira utasaidia kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi