Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sanaa Ina mchango Mkubwa katika Kuitangaza Nchi Yetu Kimataifa - Dkt. Abbasi
Nov 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi, WUSM - Bagamoyo

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema sekta ya Sanaa ina mchango mkubwa katika kuitangaza nchi kimataifa kupitia kazi za Sanaa zinazofanywa na Wasanii.

Dkt. Abbasi amesema hayo Novemba 12, 2022 wakiwa katika ziara ya kutembelea kisiwa cha Lazy Lagoon kilichopo Wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya Tamasha la 41 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambalo linafanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zainabu Abdallah ambapo wamewaongoza wasanii na wadau wa sekta za Utamaduni na Sanaa kutembelea kisiwa cha Lazy Lagoon kilichopo Wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya Tamasha la 41 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.

Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa kisiwa cha Lazy Lagoon kina mandhari nzuri na kusisitiza kuwa waandaji wa tamasha hilo wamejipanga kuionesha dunia kuwa pamoja na burudani, utamaduni na sanaa, wana fursa pia kuonesha dunia vivutio vya utalii vilivyopo katika Wilaya ya Bagamoyo.

“Sanaa ni kielelezo kikubwa sana cha kuitangaza nchi. Kwa hiyo tumekuja na wazo la kubuni kila mwaka wakati wa tamasha hili tuwe tunawapeleka wageni wetu katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, kuanzia mwaka jana tumeanza kuyaonesha wageni wetu kwa kutembelea hifadhi yetu ya Saadani, na mwaka huu tumekuja hapa kisiwa cha Lazy Laggon. Hii imechagizwa na filamu ya Royal Tour” amesema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi ameongeza kuwa ziara ya kutembelea kisiwa cha Lazy Lagoon ni mwendelezo wa filamu ya Royal Tour ya kuitangaza nchi na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhe Samia Suluhu Hassan za kuitangaza nchi kimataifa.

“Tupo hapa tumetulia kweli, eneo la kisiwa cha Lazy Lagoon limetulia na linaweza kutumika kwa kila aina ya michezo ya baharini. Wageni wengi, wawekezaji na wadau mbalimbali waje hapa, eneo linafikika kupitia chuo cha Kilimo cha Mbegani miundombinu inaruhusu watu wanaotembelea eneo hili”, amesema Dkt. Abbasi.

Ndiyo maana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akizindua tamasha la 41 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Novemba 11, 2022 mjini Bagamoyo alisema sekta ya burudani kupitia Sanaa na Utamaduni ni uchumi.

Kulingana na takwimu zilizopo hapa nchini, sekta ya burudani ndiyo sekta inayokua kwa kasi kuliko sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 katika mwaka 2021 na ina waajiri vijana wengi na inaweza kutengeneza matajiri wengi kama vipaji vya wasanii vitaendelezwa na inasaidia kuitangaza nchi yetu kwa lugha adhimu ya Kiswahili kupitia kazi za wasanii mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Zainabu Abdallah amesema Mji wa Bagamoyo unakua kwa kasi kiuchumi ukichagizwa na miundombinu imara inayojengwa na Serikali ikiwemo daraja jipya la Wami ambalo linaunganisha wilaya hiyo na mikoa ya kaskazini ya Tanga, Kilimajaro na Arusha pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.

“Serikali imeweka jitihada kubwa kuutangaza mji wa Bagamoyo kama mji wa kihistoria na mji wa kiutalii, ni lazima tuyaweke mazingira safi na salama ili yaweze kuwavutia wageni wanaokuja kutembelea na kuwekeza katika mji wetu”, amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Zainabu.

Bi. Zainabu ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mipango ya kuufungua mji huo na kuunganisha na mji wa Zanzibar kwa kujenga gati ya Bagamoyo eneo la saadani ili kurahisisha usafiri katika miji hiyo.

Aidha, Bi. Zainabu amesema kuwa Serikali na Umoja wa Mataifa wanaendelea kujenga kingo ya bahari kwa ukuta ambapo kwa upande wa Bagamoyo utaanzia Saadani hadi Mbweni Dar es Salaam pamoja na maeneo ya pwani yote kuanzia Tanga, Dar es Salaam, Lindi hadi Mtwara.

Ziara hiyo imejumuisha pia Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiongozwa na Mhe. Hamis Taletale na Mhe.  Husna Sekiboko, wasanii kutoka Zambia, Waandishi wa Habari pamoja na wadau wa Sekta za Utamaduni na Sanaa ambao wanashiriki Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo ambalo linafanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 10 hadi 12, 2022.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi