Idadi ya Watalii waliongia nchini katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2023 imeongezeka hadi Watalii 1,131,286 ikilinganishwa na Watalii 900,182 walioingia nchini katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo Oktoba 9, 2023 Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Bw. Daniel Masolwa amesema Ongezeko hilo la Watalii limesababishwa na Filamu ya Royal Tour iliyotangaza vivutio vya Tanzania Kimataifa.
"Nchi zilizoongoza kwa kuleta Watalii wengi ni pamoja na Marekani Watalii 84,541, Ufaransa 72,009, Ujerumani 57,798, Uingereza 51,505 na Italia 51,056", ameeleza
Masolwa
Amesema kwa mwezi Agosti pekee, idadi kubwa ya Watalii walioingia nchini walitoka Italia 14,986, Marekani 14,416, Ufaransa 11, 997, Uingereza 9,852 na Ujerumani 9,161.
Kwa upande wa nchi za Afrika, Nchi ya Kenya iliongoza kwa kuleta Watalii 128,753 walitembelea Tanzania, Burundi 69,505, Zambia 38,394, Rwanda 37,269, Uganda 28,594.
Sanjari na hilo, Masolwa amesema kuwa katika kipindi cha Agosti 2023 pekee nchi za Afrika zilizoongoza kuleta Watalii nchini ni Kenya 18,550, Burundi 12,310, Zambia 6,649, Rwanda 5,124 na Uganda 4,052.
Aidha, Masolwa amesema kuwa Sekta ya Utalii ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni nchini.
Taasisi na Kampuni zinazotoa huduma kwa watalii zinatakiwa kuendelea kuimarisha huduma zake ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza utalii.