Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imewezesha kuweka historia kwa kufadhili mradi wa umeme wa maji wa Ijangala kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuwanufaisha zaidi wa wananchi 4,500 wa vijiji nane vya wilayani Makete.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd, kampuni inayomiliki Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala, Bw. Elikana Kitahenga amesema tayari mchakato wa kuingizwa kwenye gridi umeanza rasmi baada ya kukamilika ujenzi wa kituo hicho.
Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kwa sasa una uwezo wa kuzalisha KiloWati 360 ambapo kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa kampuni ya Nishati Lutherani (DKK) Investment Ltd itaanza kuuza umeme huo kwa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO).
Akiongea na Wanahabari hivi karibuni Bw. Kitahenga amesema kuwa REA imetoa zaidi ya millioni 900 kwa awamu tatu katika kufadhili ujenzi wa mradi huo.
Amesema kukamilika kwa hatua hii ya mradi huo kwenye Gridi ya Taifa, kumetokana na uwezeshaji wa REA ambapo mwaka 2013, Mradi huo ulipokea awamu ya kwanza, shilingi milioni 133 na baadae mwaka 2016 Mradi ulipokea shilingi milioni 426 na awamu ya tatu, wanatarajia kupokea shilingi milioni 437.
Amesema mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa vijiji vya Masisiwe, Tandala, Ikonda, Usagatikwa na Ihela kwa kupata umeme wa uhakika utatokana na Mradi wa chanzo cha maji wa Ijangala.
Akieleza kuhusu tukio la kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa, Mshauri Elekezi wa Mradi huo wa Ijangala, Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) amesema kazi imefanywa vizuri na Wakandarasi wanne na kuongeza kuwa zoezi la kuunganisha kituo hicho na Gridi ya Taifa litakamilika ndani ya wiki moja.