Na. Tiganya Vincent, RS – TABORA.
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeaagiza Maofisa Ugani wote kuhakikisha wanasaidia wakulima wa mahindi kukabiliana na ugonjwa na Mahindi wa bungua bua(rusomi) ambayo umeanza kushambulia mahindi kwa kasi kubwa mkoani humo.
Agizo hilo limetolewa jana wilayani Kaliua na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akikagua mashamba ya pamba na mahindi ili kuona kama wakulima wa pamba wamezingatia Sheria ya Pamba inayotaka kulima kwa kufuata kanuni za kilimo bora.
Alisema kuwa tatizo hilo lisipotatuliwa linaweza kusababisha mavuno kwa wakulima kuwa mabaya na kuwa tishio la njaa katika maeneo mbalimbali.
Mwanri aliwataka Maofisa Ugani kuhakikisha wanaeleza wakulima dawa ambayo inaweza kukabiliana na tatizo hilo ili mahindi yasiendelee kuathirika.
“Wakulima wetu wamelima sana na mvua zinaoonyesha kuwa nzuri mwaka huu…tatizo ambalo nimeliona ni mahindi mengi kuanza kushambuliwa …ni vema tuwasaidie kuwaeleza wakulima sehemu ya kupata dawa zitakazowasaidia kuokoa mahindi yao”alisema Mwanri.
Naye Mshauri wa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Modest Kaijage alisema tatizo la bungua bua mara nyingi ujitokeza katika mahindi ambayo yamepandwa katika mvua za mwisho, lakini safari hii umeanza mapema.
Alisema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo katika mahindi mkulina anaweza kutumia dawa inayojukilikana kama ‘Endosulfan Thiodan dust’ ambayo itasaidia kumaliza tatizo hilo shambani.
Kaijage alitoa wito kwa Maafisa Ugani wa Vijiji na Kata kuhakikisha wanawatembelea wakulima na kuwahimiza kununua dawa ili waweze kuokoa mahindi yao yasishambuliwe zaidi.