Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora: Ma-Ded Nunueni Vifaa Vya Kupimia Ubora wa Udongo Ili Kuwasaidia Wakulima
Aug 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Tiganya Vincent, RS-Tabora

SERIKALI   imewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa na Halmashauri kuhakikisha wanawanulia Maafisa Ugani vifaa vya kupimia ubora wa udongo (soil kits) kwa ajili ya kuwawezesha kutoa huduma ya ushauri kwa wakulima ili waendeshe kilimo kulingana na hali ya udongo wa eneo husika.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifunga mafunzo ya siku saba ya Maafisa Ugani kutoka Halmashauri zinazolima zao la tumbaku kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa huduma nzuri kwa wakulima.

Alisema kuwa vifaa hivyo ni lazima vinunuliwe angalau vichache vya kuanzia ili Maafisa Ugani katika ngazi za kuanzia kijiji hadi kata waweze kuwasaidia wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo ikiwemo mbolea katika udongo husika kwa ajili kuwafanya wazalishe mazao mengi.

Mwanri aliongeza kuwa wakulima wamekuwa hawapati mafanikio wakati mwingine kwa sababu ya kukosa wataalamu wa kuwashauri jinsi ya kuendesha kilimo kulingana na udongo uliopo katika maeneo yao pamoja na matumizi sahihi ya pembejeo kulingana na hali halisi ya udongo.

“Vifaa hivyo vitasaidia wao kujua ni virutubisho gani vinapungua katika udongo na hivyo waweze kumshauri mkulima jinsi ya kuongeza virutubisho hivyo ili apate mafanikio na kuachana na kilimo cha kukisia katika matumizi ya pembejeo”alisisitiza Mkuu wa Mkoa huyo.

Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Mkoa ameziagiza Halmashauri zote zinazolima tumbaku na kupata mapato kutokana na zao hilo kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko Maalumu wa kushughulikia tatizo la usafiri kwa Maafisa Ugani ili waweze kuwafikia wakulima kirahisi na kuwapa ushauri sahihi unawawezesha kusonga mbele.

Alisema kuwa baadhi ya Kata zina maeneo makubwa ambayo bila usafiri wa uhakika inakuwa vigumu kwa Maafisa hao kuwafikia wakulima kwa wakati ili kuwasaidia kutoa ushauri unaowasaidia kuzalisha kwa tija.

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha Kilimo Tumbi Kasele Steven alisema kuwa Mafunzo hayo ya siku saba kwa Maafisa Ugani hao yamekuwa ni muhimu sana kwani wamepata elimu ambayo imewawezesha kuwa na uelewa wa kutosha juu ya zao hilo kwa sababu baadhi yao wakati wanasoma vyuoni hawakupata mafunzo kuhusu zao la tumbaku.

Alisema kuwa hivi sasa Maafisa Ugani hao watakuwa karibu sana na wakulima kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo ni Maafisa Ugani wa Kampuni za Tumbaku pekee ndio waliokuwa wakimhudumia mkulima wa tumbaku na kukosa msaada wa Wataalamu wa Serikali.

Steven aliongeza kuwa Maafisa Ugani hao wamejifunza juu ya aina na sifa za mbegu bora za tumbaku, uandaaji na utunzaji wa vitalu, maandalizi ya shamba, utunzaji wa shamba, uvunaji wa tumbaku, ukaushaji wa tumbaku, uchambuzi na upangaji madaraja ya tumbaku na Sheria na Kanuni za kilimo cha tumbaku.

Baadhi ya Wahitimu wa Mafunzo hayo wameiomba Serikali kuhakikisha kuwa Vyuo vyote wa Mafunzo ya Kilimo nchini vinakuwa na mitaala ya mazao makuu ya biashara ili kuwapa wachuo uelewa wa pamoja kuhusu mazao.

Walisema Chuo kinachofundisha zao la tumbaku ni Tumbi pekee hivyo kuwa vigumu kwa Afisa Kilimo ambaye hakupitia katika chuo hicho kuwahudumia wakulima wa tumbaku wanapopelekwa Mkoani humo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa aliyoyatoa alipofanya ziara mkoani hapo ya kutaka Maafisa hao wapatiwe mafunzo na waende kuwasaidia wakulima wa tumbaku badala ya kuwaachia wa Kampuni zinazonunua Tumbaku pekee ndio wahudumie mkulima wa tumbaku.

Katika kutekeleza agizo hilo Maafisa Ugani 114 wa Mkoa wa Tabora ambao wanatoka Wilaya za Sikonge, Nzega, Uyui, Manispaa ya Tabora, Urambo, Kaliua na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora wamehitimu na kupata vyeti vya ujuzi katika kusimamia zao la tumbaku.

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi