Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora: Asiyetaka Kwenda na Kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano Aachie Ngazi
Jan 13, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Tiganya Vincent - RS Tabora

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imetaka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ambao wamechoshwa na ufanyaji kazi kwa kuzingatia kasi ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandika barua za kuacha kazi ili kuwapisha ambao wataweza kuendana na kasi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kufuatia baadhi yao kutoroka zoezi la upandaji miti na wengine kushindwa kutekeleza majukumu yao katika zoezi hilo.

Alisema kuwa wapo watu wengi ambao wanahitaji kufanyakazi lakini hawana fursa hiyo, kama mtu anaona kazi zinazotolewa na viongozi ni bughuza kwake ni vema akajiondoa kwa hiari yake kabla hajachukuliwa hatu ikiwemo kuondolewa.

Mwanri alisema kuwa haiwezekani mtumishi wa umma akachagua kazi za kufanya na kutofanya kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maelekezo ya barua yake ya ajira.

“Mlipopata barua zenu za ajira zilikuwa zinaeleza kuwa zinaorosha kazi ambazo mtafanya na kumalizia kuwa na kazi nyingine ambazo utapangiwa na viongozi wao, na kazi hizo ni pamoja na kupanda miti” alisema Mwanri.

Alisema kuwa haiwezekani Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaagiza kila Mkoa na kila Wilaya na kila kijiji kipande miti kisha wanatokea watumishi wanakaidi kwa kudai kuwa sio sehemu ya majukumu.

Mwanri alisema kuwa kama Mtumishi wa Umma anaona kuwa upandaji miti kwake sio jukumu lake ni vema akaandika barua na akaondoka kwa amani ili aende kwa mwajiri mwingine anayeona anamfaa.

Alisema kuwa suala la kupanda miti ni kila mkazi wa Tabora wakiwemo watumishi wa umma na wananchi.

Mwanri alisema kuwa miti si mali ya Mkuu wa Mkoa , wala Mkuu wa Wilaya bali ni kwa ajili ya faida ya wakazi wote wa Tabora.

Alisema kuwa kukitokea jangwa hakutamuathiri Mkuu wa Mkoa au viongozi pekee hata wale wanaojifanya hawataki kupanda miti.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi