Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora Apiga Marufuku Usafirishaji Tumbaku Nje ya Wilaya.
May 23, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent – RS Tabora

Mkuu wa  Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amepiga marufuku usafirishaji wa  tumbaku kutoka Wilaya moja kwenda nyingine ili kudhibiti utoroshaji unaotarajiwa kufanya na baadhi ya wakulima wasio waaminifu ambao hadi hivi sasa wamekaidi agizo la Waziri Mkuu la kuwataka wakulima wote kuuza  tumbaku yao kupitia Vyama vya Msingi vilivyopo katika maeneo yao.

Marufuku hiyo inafuatia wakulima wa kujitegemea (IF) zaidi ya 16 kutoka Wilaya ya Urambo na Uyui kukataa kujisajili katika Vyama vya Msingi na hivyo kutoonyesha kuwa watauzia tumbaku yao kupitia Chama gani cha Msingi.

Mkuu wa Mkoa huyo alitoa agizo hilo jana mjini Tabora wakati wa kikao cha wadau wa tumbaku, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa , ambapo pamoja na mambo mengine kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania kimejadili tarehe ya kuanza kwa  masoko ya tumbaku ambayo yataanza siku ya Ijumaa wiki hii (26.5.2017) katika meneo mbalimbali.

Alisema kuwa Serikali iliamua wakulima wote kuuzia tumbaku yao kupitia Vyama vya Msingi katika maeneo yao na sio vinginevyo ili kuepuka watu wanatumia mwanya wa kujitegemea kuwarubuni  tumbaku ya wakulima wadogo wadogo walipo katika vyama vya msingi na kuwauzia baadhi ya tumbaku yao na kusababisha madeni katika vyama vyao vya Msingi.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa hadi hivi sasa baadhi ya wakulima hao wamekata kujisajili katika Vyama vya Msingi vilivyopo katika maeneo yao na hata kwingine ni ishara tosha kuwa wanampango wa kutorosha tumbaku hiyo kwenda kuuzia wanakujua kinyume na agizo la Waziri Mkuu.

Alisisitiza kuwa yeye akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa  hawezi kukubali watu wakaidi agizo la Waziri Mkuu kwa nia ya kutaka kuwanyonya wakulima wengine.

Kufuatia hali hiyo aliagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa , Wilaya kushirikiana na Watendaji ngazi za chini na kuwakamata wao na mizigo yote itakayokuwa inasafirisha nje ya eneo la Chama cha Msingi la Mkulima anapokaa kama bidhaa hiyo haijanunuliwa na kupata hati inayotambulika na Bodi ya Tumbaku ya Tanzania (TTB) na wanunuzi rasmi wa tumbaku wenye vibali vya kufanya kazi hiyo mkoani Tabora.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alitoa angalizo kwa vyombo vyote vinavyotumika kusafirisha tumbaku kutoka eneo moja kwenda jingine kuhakikisha mzigo waliopakia katika magari unavibali vyote baada ya ununuzi katika soko kupitia Chama cha Msingi ili kuepuka usumbufu na kuchukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza Wakurugenzi Watendaji, Maafisa Ushirika,Wanasheria na Wawakilishi wa Benki za CRDB na NMB kukaa meza moja na kuangalia uwezekano wa kuweka makubaliano ambayo yatawahakikisha wakulima wote wa tumbaku ambao walilima kwa kutumia pembejeo zao wasiathirike na makato ya madeni ya wakulima wanaodaiwa.

Alipendekeza kuwepo na Akaunti mbili, moja ni ile inayomlinda mkulima wa aliyejitegemea na nyingine ya wakulima ambao wanadaiwa ili kila mtu apate haki kulingana na alivyojiandaa katika kilimo hicho.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa hakuna atakayenyimwa haki yake kwa sababu ya watu wengine.

Hata hivyo wadau hao wa tumbaku walisema hakuna  haja ya kuwa na akaunti mbili badala yake Benki zinaweza kuweka utaratibu mzuri wa utambuzi wa mtu aliyelima kwa kujitegemea na kumpa fedha zake zote na wale wanaodaiwa wakaendelea na utaratibu wanaoutumia.

Walisema kuwa hatua itawasaidia wakulima waliojitegemea na kuamua kuuzia tumbaku yao kupitia vyama vya msingi kupata haki yao bila kuchelewa kwa kusubiri deni la Chama cha Msingi limalizike kwanza ndio walipwe.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara amesema kuwa baadhi ya matatizo na migogoro katika zao la tumbaku yamesababishwa na maslahi binafsi ya baadhi ya watumishi wakiwemo Maafisa Ugani, Maafisa Ushirika , Wafanyakazi wa Mabenki na watumishi wengine wanaojihusisha ununuzi usio halali wa zao hilo na kilimo hicho.

Alisema kuwa watumishi hao ndio wamekuwa wakichochea migogoro na wengine kuwarubuni wakulima kwa kununua tumbaku yao kinyume cha utaratibu na kuwafanya walaze madeni.

Dkt. Ntara alisema kuwa ili zao hilo limsaidie mkulima  ni vema wataalum wakafanyakazi zao za utaalam kuliko kuwa  washindani wa wakulima na hivyo wakati kuanzisha migogoro kwa maslahi yao binafsi ili hatimaye wakulima wakate tamaa na kuanza kuuza tumbaku katika masoko yasiyo rasmi.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi