Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela amempongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Ruby International Ltd na Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Mhe. Salim Alaudin Hasham kwa kampuni yake kuwa kinara wa ulipaji kodi katika sekta ya madini.
Shigela ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika migodi ya Epanko wilayani Ulanga kwa lengo la kujionea namna shughuli za uchimbaji madini unavyofanyika.
Aidha, Shigela alipata wasaa wa kuzungumza na wafanyakazi wa migodi hiyo huku akiwasihi kuwa waaminifu ili kumpa nguvu mwekezaji huyo mzawa aendelee kutanua wigo wa uwekezaji na ajira ziweze kuongezeka.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ruby International ltd na Mbunge wa Jimbo hilo la Ulanga amesema, anajivunia kuwa ni sehemu ya kuzalisha ajira kwani kwa sasa ana wafanyakazi zaidi ya 300 na anatarajia kutanua mgodi huo ili aweze kufikia ajira 700 mpaka 1000.
Migodi ya Epanko inachimba madini ya Spinel ambayo yanatumika kutengenezea thamani mbalimbali.
Mkuu wa mkoa Martine Shigela yupo wilayani Ulanga kwa ziara ya siku mbili kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo inavyokwenda na kuhakikisha fedha za serikali zinatumika ipasavyo.
Ruby International Ltd iliibuka kinara wa ulipaji kodi katika sekta ya Madini na kukabidhiwa tuzo iliyoandaliwa na wizara ya madini katika hafla maalum ambayo Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mgeni rasmi.