Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Gabriel Azitaka Taasisi na Mashirika Kushirikana na HESLB
Oct 12, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amezitaka taasisi, mashirika na makampuni ya sekta za umma na binafsi  kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika kuwabaini wanufaika wa mikopo hiyo ili kuiwezesha Serikali kuwa na mfuko endelevu wa elimu ya juu.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao kazi cha 10 cha Maafisa Madawati ya Mikopo katika taasisi za Elimu ya Juu kinachoendelea Jijini Mwanza leo Jumatatu Oktoba 11, 2021, Mhandisi Gabriel alisema ni wajibu wa wanufaika kurejesha mikopo hiyo, kwani HESLB imewawezesha kupata ujuzi wa kitaaluma na kuweza kujiinua kiuchumi kupitia Elimu.

“Tunatambua kuna idadi kubwa ya wataalamu waliowezeshwa na HESLB kupata mikopo ya elimu ya juu, ni wajibu wetu kuhakikisha tunarejesha fedha hizo ili ziweze kuwanufaisha Watanzania wahitaji, Ofisi yangu itashirikiana na HESLB katika kuhakikisha wanufaika waliopo katika sekta rasmi na zisizo rasmi wanarejesha mikopo hii” alisema Mhandisi Gabriel.

Aidha, Mhandisi Gabriel aliitaka HESLB kutumia fursa za majukwaa, mikutano na makongamano ya wadau na wanataaluma mbalimbali ili kuweza kuwabaini wanufaika  wa mikopo ya elimu ya juu, kwa kuwa hatua hiyo itaongeza kasi ya makusanyo kutoka kwa wanufaika ambao  hawajaanza kurejesha mikopo yao.

Kwa mujibu wa Mhandisi Gabriel, alibainisha kuwa Mkoa wa Mwanza umekuwa kimbilio kubwa la mikutano na makongamano ya wanataaluma mbalimbali, hivyo HESLB haina budi kuweka mikakati mahsusi ya kupata orodha ya wanufaika walioajiriwa katika makampuni, taasisi na mashirika hayo ili kuweza kuwabaini wanufaika wengi zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema HESLB kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2016/2017-2020/2021), imeendelea kuimarisha mashirikiano na wadau na kubuni mifumo mbalimbali ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika.

“Hivi karibuni tunatarajia kuzindua akaunti ya LIPA, ni akaunti maalum ya mnufaika wa mikopo, kupitia akaunti hiyo mnufaika ataweza kupata taarifa za deni la mkopo aliopatiwa na HESLB wakati wa masomo, hii itaongeza hamasa ya urejeshaji kutoka kwa wanufaika” alisema Badru. 

Akizungumzia maudhui ya kikao kazi hicho, Badru alisema kikao hicho kimeshirikisha jumla ya washiriki 150 kutoka taasisi za elimu ya juu81 za umma na binafsi, wakiwemo Maafisa Mikopo takribani 125; wawakilishi wa Serikali za Wanafunzi na Menejimenti ya HESLB.

“Maafisa Mikopo ni wadau muhimu wa HESLB, kutokana na majukumu yenu ya kuhudumia wanafunzi tumeamua kukutana nanyi ili kubadilishana uzoefu katika eneo la upangaji, utoaji na urejeshaji mikopo lakini pia kupokea maoni, ushauri na changamoto katika sehemu za kazi” alisema Badru.

Naye Meneja wa HESLB, Kanda ya Ziwa, Usama Choka alisema Ofisi yake imeendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mwanza katika juhudi na jitihada mbalimbali inazoendelea kuzifanya katika kuwabaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi