Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais wa Ethiopia Mhe. Sahle-Work Zewde Afanya Ziara ya Siku 1 Nchini Tanzania
Jan 25, 2021
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde amefanya ziara ya kikazi ya siku 1 hapa nchini ambapo amefanya mazungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake Chato, Mkoani Geita.

Baada ya mazungumzo yao, Waheshimiwa Marais hao wamezungumza na Vyombo vya Habari ambapo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Sahle-Work Zewde kwa kufanya ziara hapa nchini, na kwamba hii inaimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ethiopia ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia Hayati Haile Selassie I tangu mwaka 1963.

Mhe. Rais Magufuli amesema wamezungumzia kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao kwa sasa bado upo katika kiwango chini licha ya kuwepo ongezeko la biashara kutoka shilingi Bilioni 3.07 mwaka 2016 hadi kufikia shilingi Bilioni 13.55 mwaka 2019/20 na kuwepo uwekezaji wa miradi 13 ya Ethiopia yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 14.57 iliyozalisha ajira 567 hapa nchini.

Maeneo mengine ni kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga na utalii, ulinzi, kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia, kushirikiana mbinu za kunufaika na mazao ya mifugo hasa ikizingatiwa Ethiopia na Tanzania zinashikana nafasi ya kwanza na ya pili (mtawalia) kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na kuhakikisha Kamati ya Pamoja ya Majadiliano (JPC) inakutana haraka ili kupitia maeneo yote ya ushirikiano na kuongeza maeneo mapya.

Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari kuwaachia Wafungwa na Maabusu 1,787 wa Ethiopia wanaoshikiliwa katika Mahabusu mbalimbali hapa nchini baada ya kukamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria na ameiruhusu Ethiopia kutuma ndege wakati wowote ili kuwarejesha nyumbani kwao.

Kuhusu viwanja vya Tanzania vilivyopo Addis Ababa ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivinyang’anya kutokana na Tanzania kutoviendeleza kwa mujibu wa sheria za Ethiopia, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania imechukua hatua dhidi ya waliohusika katika upotevu wa fedha za uendelezaji wa viwanja hivyo na ameiomba Serikali ya Ethiopia kuvirejesha kwa Tanzania ili viendelezwe.

Kwa upande wake Mhe. Rais Sahle-Work Zewde amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumkaribisha hapa nchini na ameshukuru kwa kuendeleza uhusiano mzuri wa Tanzania na Ethiopia uliodumu tangu enzi za kupigania ukombozi wa Afrika.

Amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kipindi cha pili kuiongoza Tanzania na amebainisha kuwa Ethiopia ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kukuza biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais  Sahle-Work Zewde amesema Tanzania ni nchi muhimu Barani Afrika kutokana na kuhusika kwake katika masuala ya kimajumuhi ikiwemo kutafuta amani na ndio maana Ethiopia ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania.

Amepokea ombi la kurejeshwa kwa viwanja vya Tanzania vilivyonyang’anywa na Serikali ya Ethiopia kutokana na kutoendelezwa, ameshukuru kwa utayari wa Tanzania kupeleka Walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia, ameafiki ushirikiano wa Tanzania na Ethiopia katika kunufaika na utajiri wa mifugo mingi iliyopo na ameishukuru Tanzania kwa utayari wake wa kuwaachia Wafungwa na Maabusu wa Ethiopia 1,789 waliopo magerezani hapa nchini baada ya kukamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

Mhe. Sahle-Work Zewde amemaliza ziara yake na amerejea Addis Ababa nchini Ethiopia.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

25 Januari, 2021

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi