Na Immaculate Makilika - MAELEZO, Iringa
Serikali imefikia uwamuzi wake wa kutekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo Iringa ili kusaidia shughuli za biashara na utalii kwa lengo la kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Akizungumza leo wakati akiweka jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uwanja huo utakaogharimu takribani shilingi bilioni 63.7 utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa zitakazotua, ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira 150 wakati wa ujenzi wake.
"Imani yetu kuwa baada ya miezi 18 hadi 20 Iringa sasa zitatua ndege kubwa zenye idadi ya kuanzia abiria 70 na kwa vile nyie ni wazalishaji wa mazao kama vile chai sasa itakuwa rahisi kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya nchi". Amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa uwanja huo utafungua mkoa huo kwa fursa za utalii sambamba na kuendeleza maeneo ya utalii.
Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wa Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati amesema kuwa ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege utafungua fursa za kiuchumi kupitia utalii.
"Iringa ni kitovu cha utalii Nyanda za Juu Kusini, kukamilika kwa uwanja huu tunaenda kupata utalii zaidi. Pia, ujenzi wake unaenda sambamba na ujenzi wa barabara ya lami hadi katika Hifadhi ya Taifa Ruaha hivyo itakuza sekta ya utalii hapa Iringa". Amesema Kabati
Mbunge huyo ameongeza kuwa wakulima wa matunda na mbogamboga wamekuwa wakitumia Uwanja wa Ndege wa Arusha kusafirisha bidhaa zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa, Paul Walalaze amesema kuwa uwanja huo utafungua fursa za biashara katika mkoa huo.
"Uwanja huu utaongeza uwekezaji katika mkoa wetu wa Iringa na Serikali itapata mapato yake kupitia biashara zitakazofunguliwa hapa, wasafiri wengi zaidi watashuka hapa na kuondoka na hivyo Serikali itapata fedha za gharama ya kuondokea yaani departure charges" Amesema Walalaze.
Naye, Mfanyabiashara, Alif Abri amesema kuwa uwanja huo wa ndege utasaidia usafirishaji wa abiria na mizigo kwa muda mfupi kwa kuwa awali walitumia hadi saa kumi kufika Dar Es Salaam.
"Watalii sasa watashuka kwa wingi hapa na itasaidia hoteli zetu, nyumba za kulala wageni na biashara zingine kwa vile kutakuwa na mzunguko mkubwa wa fedha. Vilevile, jirani zetu wa Mkoa wa Njombe nao watatumia uwanja huu kusafirisha maparachichi kwenda sehemu mbalimbali". Amesema Abri.
Ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege unahusisha pia ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, eneo la maegesho ya ndege, ujenzi wa Kituo cha umeme, ujenzi wa uzio wa usalama na jengo la waongoza ndege.