Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Shule ya Msingi Imbele iliyojengwa katika Manispaa ya Singida mkoani Singida kwa niaba ya shule zote zinazojengwa kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) wenye thanani ya shilingi trilioni 1.5.
Raia Dkt. Samia amezindua shule hiyo leo Agosti 15, 2023, yenye thamani ya shilingi milioni 493 ambayo ni sehemu ya mradi wa BOOST, wakati wa ziara yake mkoani Singida ikiwa ni mradi wa kwanza tangu alipopowasili mkoani humo.
Amesema amezindua mradi huo kwa niaba ya miradi mingine yote kama hiyo iliyo chini ya BOOST inayojengwa nchini na itasaidia watoto waweze kupata elimu bora.
“Watoto wetu kazi yenu sasa ni kusoma kwa sababu shule nzuri mnazo na utaona kwenye mradi huu wa BOOST tumejenga kuanzia madarasa ya awali, hivyo mtoto akiwa na umri kuanzia miaka minne apelekwe hapo ili aandaliwe kuanza darasa la kwanza.
Pia ametoa rai kwa wazazi na walezi wote kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa shule na wanasoma mpaka kumaliza masomo yao na kuitaka jamii kuitunza miradi hiyo ili iweze kunufaisha vizazi vijavyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema mradi huo umeanza kutekelezwa mwaka 2021 na kwa mwaka huu wa fedha shule mpya za msingi 302 zinajengwa, vyumba vya madarasa 2,929 yakiwemo ya mfano ya Elimu ya Awali 368, matundu ya vyoo 5,131, nyumba za Walimu 41, mabweni mawili na majengo ya Utawala 302.
“Mpaka mwezi Septemba 2023 tumeshatoa shilingi bilioni 230, na shule za msingi zilizokamilika mpaka sasa ni 194, madarasa ya awali 364, madarasa ya shule za msingi 2,303 na zingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi wake,” ameeleza Mchengerwa.
Mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano utagharimu shilingi trilioni 1.5 na unalenga kuimarisha elimu ya awali na msingi nchi nzima