Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Awataka Viongozi Kuzungumza na Wananchi
Mar 30, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Georgina Misama – MAELEZO, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri, Wabunge na viongozi mbalimbali wa Kisekta nchini kuzungumza na wananchi kuhusu kero zinazowakabili.

Rais Samia aliongea hayo leo Machi 30, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma wakati akipokea Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Rais Samia alisema kwamba kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali sokoni hasa mafuta ya kula pamoja na mafuta ya petroli na diseli ambapo ni matokeo ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani.

“Wabunge na Viongozi mnaosimamia Sekta waambieni wananchi ukweli waelewe yanayoendelea duniani, vita ya Russia na Ukraine imepandisha sana bei ya mafuta na kupelekea bei ya bidhaa zote kupanda kutokana na gharama za usafiri kupanda”, alisema Rais Samia

 Aliongeza, mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani pia umechochea mfumuko wa bei za bidhaa kwa kuwa bidhaa zote zilizohifadhiwa kwenye maghala zilitumika kwa vile uzalishaji ulisimama kwa kipindi chote ambacho hofu ya COVID 19 ilikuwa juu zaidi.

“Ukiangalia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na kati, Tanzania ndio nchi yenye bei ya chini zaidi ya mafuta ambapo Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kupunguza ikiwemo kuondoa tozo lakini bado bei iliendelea kupanda kwenye soko la dunia, viongozi waelezeni haya wanachi waelewe”, aliongeza Rais Samia.

Kuhusu suala la kupanda bei ya mafuta ya kula Rais Samia aliwaagiza viongozi wenye Sekta husika kuchukua hatua stahiki kwa suala hilo ili kuhakikisha wananchi hawakosi bidhaa hiyo sokoni.

“Nawaagiza viongozi waangalie suluhu ya changamoto ya mafuta ya kula, tulisimamisha kuingiza mafuta kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani, lakini hivi sasa viwanda vyote vya ndani vimesimamisha uzalishaji, nataka viongozi wangalie kama tunaweza kuyaruhusu sasa ili wananchi wasikose bidhaa sokoni”.

Kwa upande mwingine Rais Samia alitoa maelekezo kwa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kujichunguza na kujirekebisha ili kuhakikisha majukumu ya kila Sekta yanatekelezwa kwa wakati na kwa weliedi ambapo alisema viongozi wanaohusika na kutoa maamuzi wafanye hivyo bila kupoteza muda.

“Bohari Kuu ya Madawa naitaka ifanyiwe mabadiliko makubwa kuanzia ngazi ya uongozi wa juu mpaka kwenye vitengo vyake ili tuweze kwenda mbele, huko nyuma ilishafika hatua ya kupata tenda kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), lakini hatua iliyofikiwa sasa hata ndani watu wanalalamika hawapati huduma, kwa vile SADC bado wana imani nasi turekebishe ili twende mbele”, alisema Rais Samia.

Taasisi nyingine zilizoguswa na ripoti hiyo ni pamoja Mfuko wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Sekta ya  Afya na Maji ambapo Rais Samia aliwataka Wabunge kufanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa kwenye ripoti hiyo kwa haraka na kutoa majibu kwa wananchi pindi watakapoenda bungeni.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi