Na Lilian Lundo - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu kusimamia fedha za UVIKO-19 ili zifanye matumizi vile inavyotakiwa.
Rais Samia amesema hayo Januari 4, 2022 Ikulu, Jijini Dar es Salaam, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa matumizi ya fedha za UVIKO-19 shilingi Trilioni 1.3.
"Maneno nje ni mengi sana, zinaliwa, wanampango hawa wa kuzila, nendeni kaonyesheni kwamba hatuna nia hiyo. Nia yetu ni kupeleka huduma kwa Wananchi," alisema Rais Samia.
Ameendelea kusema kuwa, fedha hizo zinaingia kwenye manunuzi mengi, ambapo kuna maeneo mengine mikataba imesainiwa na maeneo mengine hawajasaini mikataba. Hivyo amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu kusimamia fedha hizo kama ilivyokusudiwa.
Aidha, ameiagiza Wizara ya Maji kutumia fedha hizo za UVIKO-19 kuagiza mitambo ambayo imefikia viwango vinavyotakiwa ili mitambo hiyo itumike kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imeidhinishiwa Shilingi bilioni 512,143,513,448 ambapo shilingi bilioni 240 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12,000 ya shule za sekondari, shilingi bilioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule shikizi za msingi na shilingi bilioni 4 ni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Pia ameeleza kuwa, shilingi 203,143,513,448 zimeidhiniwa kwa ajili kuimarisha afya msingi. Aidha, shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga.
"Mradi huu utaleta faida mbalimbali kwa mfano, fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya sekondari zitasaidia wanafunzi wote 907,803 (kwa ufaulu wa asilimia 81.97) waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kuanza shule mara moja badala ya kuwa na awamu tatu kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita.
Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2021 ni 422,403 ambao waliacha madarasa 8,448 na wanafunzi wa kidato cha kwanza walihitaji madarasa 18,156 na hivyo kuwa na upungufu wa madarasa 9,708 na tunakushukuru Mhe. Rais, ulitupatia madarasa 12,000 kwa kuwa makadirio yalifanyika kwa ufaulu wa asilimia 90 na hivyo tuna madarasa ya ziada 2,292 ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi wa vidato vingine yaani kidato cha II - IV," alifanunua Waziri Ummy.
Aidha amesema kuwa, jumla ya shilingi 203,143,513,448 zimeidhiniwa kwa ajili kuimarisha afya msingi. ikiwamo shilingi bilioni 108 za kujenga majengo ya huduma ya dharura na wagonjwa mahututi pamoja na vifaa vyake, shilingi bilioni 21.096 zimeidhinishwa kwa ajili ya ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza hewa tiba ya oksijeni katika hospitali 26 za Wilaya.
Ameendelea kusema kuwa, shilingi bilioni 22.1 zimetolewa kwa ajili ya kuimarisha huduma za uchunguzi na tiba za mionzi katika vituo vya afya na hospitali za wilaya 65, shilingi bilioni 23.525 kwa ajili kuboresha utoaji wa huduma za chanjo na uratibu wa huduma za afya.
Vilevile ameeleza kuwa, shilingi milioni 900 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kutoa huduma za dharura katika Mkoa wa Kigoma Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, shilingi bilioni 13.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 150 za watumishi wa afya zenye uwezo wa kuchukua familia 3 kila nyumba moja kwenye maeneo yenye mazingira magumu, pamoja na shilingi bilioni 4.9 kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi wa afya, ufuatiliaji na ajira za muda kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya.