Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Awashukuru Viongozi wa Dini Ushiriki wa Sensa
Oct 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Ahmed Sagaff, MAELEZO


Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewashukuru viongozi wa dini zote nchini kwa kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wafuasi wao kuhusu Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti, 2022.


Akizungumza hivi karibuni katika Baraza la Maulid lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Nchi amesema viongozi wa dini kupitia taasisi zao, wamekuwa wakiiunga mkono Serikali katika jitihada za kuwaletea maendeleo Watanzania.


“Natoa shukrani maalum kwa taasisi mbalimbali za dini kwa ushirikiano mnaoutoa kwa Serikali katika nyanja mbalimbali, tunathamini sana michango na huduma zenu katika jamii katika nyanja za afya, elimu maji na maeneo mengine tofauti tofauti yakiwemo hata ya kudumisha amani na utulivu na kuhimiza utekelezaji wa Sera za Serikali.


“Ni hivi karibuni tu tumeshuhudia viongozi wa dini wote kwa umoja wenu mkiwahimiza wafuasi wenu wajikinge na maradhi ya UVIKO-19 lakini mifano mengine ni lile swala la Sensa ambalo viongozi wa dini wote kwa umoja wenu mlisimama na kuwaeleza waumini kuhusu sensa”, ameeleza Rais Samia.


Sambamba na hayo, Mkuu wa Nchi amesema Serikali itashirikiana na viongozi wa dini katika kuwaelimisha Watanzania kujikinga na Ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa hivi karibuni kwenye nchi jirani ya Uganda.


Hafla ya Baraza la Maulid ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Mhe. Abdulrahman Kinana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla na viongozi wa madhehebu ya dini zote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi