Na Grace Semfuko, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri aliowaapisha leo Oktoba 03, 2022, kuheshimu Katiba, kujua mipaka na kutunza siri za Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao.
Mhe. Rais ametoa maelekezo hayo ya kiuongozi baada ya kuwaapisha Mawaziri hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo pia amewataka kuwa sehemu ya maamuzi ya Serikali na si kujiweka nyuma.
“Mnaposema nitailinda, nitaiheshimu na kuitetea, ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Muungano wenye pande mbili, mtatumika sehemu zote sawa kwa jinsi Katiba ilivyogawa majukumu.
Lingine ni kujua mipaka, Mamlaka na Mamlaka uliyowekewa ina ukomo wake, unapotaka kuvuka lazima upate ruhusa ya Mamlaka ya juu, lazima mjue na pia siri, siri imesemwa kwenye Baraza la Mapinduzi, umeitwa ukaelezwa, hiyo ni siri, na unapotaka kuisema au kuifanyia kazi ujue jinsi ya kuitumia hiyo siri kufanya kazi” ameeleza Rais Samia na kuwataka Mawaziri hao kutunza viapo vyao kwa kuitumikia nchi na wananchi wake.
Aidha, amewaambia Mawaziri hao kutambua kuwa jambo linaloamuliwa na Serikali ni jambo la Waziri husika na alifanyie kazi ipasavyo na kwamba hawapaswi kukwepa majukumu yao.
“Jambo linaloamuliwa na Serikali wewe kama Waziri ni lako na unatakiwa ulibebe ukalifanyie kazi kwa misingi ile uliyoelezwa, huwezi kusema nimeelekezwa hivi, mimi sikutaka hivi, lakini imebidi nifanye hivi kwa sababu nimeelekezwa, huwezi kujitoa”, amesema Mhe. Rais.
Mhe. Rais Samia amewaapisha Mawaziri watatu ambapo ni Mhe. Stergomena Laurance Tax kuwa Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Mhe. Angela Kairuki ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum na pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).