Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakazi wa Singida Kaskazini kwamba upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo hilo utafikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo mkoani Singida baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Mhe. Abeid Ighondo Ramadhani kumueleza kwamba upatikanaji wa huduma hiyo umefikia asilimia 70 tu.
"Baada ya miaka miwili tutakuwa tumefikia asilimia 85 kama tulivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025," ameeleza Mkuu wa Nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amewaarifu wananchi wa jimbo hilo mpango wa Serikali katika kuhakikisha inatekeleza maelekezo ya Ilani.
"Serikali imedhamiria kwamba sehemu inayohitajika kuchimba kisima tutachimba kisima, na sehemu inayohitajika kuchimba bwawa tutachimba bwawa ili kutimiza dhamira ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani," amedokeza Waziri Aweso.
Awali, Mhe. Ramadhani alimueleza Rais Samia kwamba uongozi wa Jimbo la Singida Kaskazini unashirikiana vyema na Wizara ya Maji katika kushughulikia ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji mbalimbali.
"Tunashukuru sana kwa kutuletea mtambo wa kuchimba visima, mpaka sasa katika jimbo letu kuna visima 15 tu ambavyo vimeshachimbwa katika vijiji mbalimbali," amesema Mhe. Ramadhani.
Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia amekuwa akitekeleza miradi mbalimbali huku akiwahimiza wasimamizi wa miradi hiyo kuwa waadilifu ili iweze kukamilishwa kwa ufanisi kama ilivyokuwa katika uongozi wa mtangulizi wake.