Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa miezi sita kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha changamoto ya mgao wa umeme inamalizika nchini.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni.
"Tuna janga la kwetu sote linalotokana na kutofanya ukarabati wa mitambo yetu ya umeme kwa muda mrefu, sasa umeme unasumbua lazima tufanye mgao, wakati wataalamu wanakarabati mitambo ya kufua umeme huo," amesema Rais Mhe. Dkt. Samia.
Agizo la Rais Samia limekuja baada ya kumteua Meja Jenerali, Paul Kisesa Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO pamoja na kumteua Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo.
Aidha, Rais Samia amevunja Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kumteua Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Gideon Kingu kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.