Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa tarehe 23 Agosti ambayo ni siku ya Sensa na Makazi ya Watu iwe ni siku ya mapumziko.
“Ninayo furaha kuwajulisha wajumbe wa kikao hiki kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti iwe ni siku ya mapumziko ili Watanzania wawepo majumbani, waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo husika,” amesema na kuamsha shangwe ukumbini.
Waziri Mkuu ametoa tamko hilo leo (Jumatano, Agosti 17, 2022) kwenye kikao cha saba cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema kutokana na uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais, anaamini zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litaenda vizuri kama lilivyopangwa.
Mapema, Waziri Mkuu alipokea vishikwambi 600 kutoka kwa Balozi wa Korea Kusini, Mhe. Kim Sun Pyo vyenye thamani ya Shilingi milioni 202. Pia alipokea fulana 1,759 zenye ujumbe wa kuhamasisha sensa zenye thamani ya Shilingi milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Serikali wa Benki ya NMB, Bw. William Makoresho ambaye alikabidhi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa benki hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho walijulishwa kwamba utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebainisha kuwa uelewa wa wananchi kuhusu zoezi zima la sensa umefikia asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 96 ya Juni, 2022.