Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Atangaza Baraza Jipya la Mawaziri 27, Sura Mpya Zatawala
Nov 18, 2025
Rais Samia Atangaza Baraza Jipya la Mawaziri 27,  Sura Mpya Zatawala
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mawaziri pamoja na viongozi wa dini mara baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 18 Novemba, 2025.
Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza Baraza jipya la Mawaziri lenye jumla ya Wizara 27 litakalohudumu katika kipindi cha miaka 5 ya uongozi wake likiwa na Wizara Mpya ya Vijana na sura mpya za mawaziri walioingia kwa mara ya kwanza.

Akitangaza baraza hilo leo Novemba 17, 2025 Ikulu, Chamwino, Dodoma, Rais Samia ameunda  Wizara mpya ya  Maendeleo ya Vijana ikiongozwa na Mhe. Joel Arthur Nanauka chini ya Ofisi ya Rais huku akiiboresha Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na kuwa Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano ambayo itafanya kazi ya kuleta maridhiano nchini ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa leo na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete ambaye ameteuliwa kuwa Waziri, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora na Naibu wake Mhe. Regina Ndege Qwaray, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Naibu wake Mhe. Pius Stephen Chaya.

Wengine ni Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira na Naibu wake Mhe. Dkt. Festo John Dugange. Kwa upende wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Wenye Ulemavu amemteua Mhe. William Vangimembe Lukuvi kuwa Waziri na Mhe. Ummy Nderiananga kuwa Naibu Waziri.

Aidha, Rais Samia amemteua Mhe. Deus Clement Sangu kuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano na Mhe. Rahma Riadh Kisuo kuwa Naibu wake huku Prof. Riziki Silas Shemdoe akiteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akiwa na Manaibu Mawaziri wawili ambao ni Mhe. Reuben Nhamaniko Kwagira upande wa elimu na Dkt. Jafar Rajab Seif upande wa Afya.

Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Rais Samia amemteua Mhe. Balozi Khamis Musa Omar kuwa Waziri wa Fedha akiwa na Manaibu Mawaziri Wawili ambao ni Mhe. Laurent Deogratius Luswetula na Mhe. Mshamu Ali Munde. Pia amemteua Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuweka Manaibu Mawaziri katika wizara hiyo ambao ni Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe na Mhe. James Kinyasi Millya.

Aidha, Rais Samia amemteua Mhe. Boniface Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu wake Mhe. Denis Lazaro Londo. Kwa upande wa Wizara ya Kilimo Rais Samia amemteua Mhe. Daniel Chongolo kuwa Waziri wa Kilimo na Mhe. David Ernest Silinde kuwa Naibu Waziri.

Mawaziri wengine ni Mhe. Jumaa Hamidu Aweso ambaye amebaki kwenye wizara yake ya awali ya Maji na Naibu wake Mhe. Kundo Andrea Mathew huku Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akimteua Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyasaho.

Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi amemteua Mhe. Abdallah Hamis Ulega kuwa Waziri na Mhandisi Godfrey Msongwe  Kasekenya kuwa Naibu Waziri. Hali kadhalika katika eneo la uchukuzi Mhe. Rais amemteua Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kuwa Waziri na Mhe. David Mwakiposa Kihenzile kuwa Naibu Waziri huku Wizara ya Viwanda na Biashara akiwateua Mhe. Judith Salvio Kapinga kuwa Waziri na Mhe. Patrobas Paschal Katambi kuwa Naibu Waziri.

Kwa upande wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Rais amemteua Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki kuwa Waziri na Mhe. Switbert Zacharia Mkama kuwa Naibu Waziri. Katika eneo la Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum, Rais Samia amemteua Mhe. Dorothy Onesphoro Gwajima kuwa Waziri na Mhe. Maryprisca Winfred Mahundi kuwa Naibu Waziri.

Katika Sekta ya Afya, Rais Samia amemteua Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa kuwa Waziri wa Afya na Mhe. Dkt. Frolence George Samizi kuwa Naibu Waziri wa Afya. Aidha, Rais Samia amemteua Prof. Adolf Faustine Mkenda kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mhe. Wanu Hafidh Ameir kuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo.

Kwa Upande wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rais Samia amemteua Dkt. Leonard Douglas Akwilapo kuwa Waziri na Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya kuwa Naibu wake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiwateua Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri na Mhe. Hamad Hassan Chande kuwa Naibu Waziri.

Katika kuendeleza Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rais Samia amemteua Prof. Palamagamba John Kabudi kuwa Waziri huku akimpatia Manaibu Waziri wawili ambao ni Mhe. Hamisi Mwinjuma na Mhe. Paul Christian Makonda. Aidha, kwa upande wa Sekta ya Madini amemteua Mhe. Anthony Peter Mavunde kuwa Waziri na Mhe. Dkt. Steven Lemomo Kiruswa kuwa Naibu Waziri.

Katika eneo la Sekta ya Nishati, Rais Samia amemteua Mhe. Deogratius Ndejembi kwa Waziri na Mhe. Salome Wycliffe Makamba kuwa naibu wake huku Wizara ya Katiba na Sheria akimteua Mhe. Juma Zuberi Homera kuwa Waziri na Mhe. Zainabu Athman Katimba kuwa Naibu Waziri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi