Na Paschal Dotto-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Vyama vya Siasa vinatakiwa kuzingatia jinsia katika kutekeleza majukumu yake ya uongozi hasa wakati wa chaguzi nje na ndani ya chama ambapo ameshukuru Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia nchini kuibua hoja hiyo muhimu.
Akizungumza katika Hafla ya kupokea Ripoti ya Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia nchini ambayo imewasilishwa leo Oktoba 21, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia alisisitiza uwepo wa usawa wa kijinsia katika vyama vyote nchini.
“Nakubaliana na asilimia 40 ya mambo ya jinsia ndani ya Vyama vya Siasa kuanzia kwangu lakini na wengine twende katika misingi hiyo ili tuwawezeshe wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za Vyama vya Siasa hasa kwenye ngazi ya uongozi”, Alisema Rais Samia.
Rais Samia pia alisema kuwa ukatili wa kijinsia kwenye vyama hivyo ni jambo ambalo anakubaliana nalo na Serikali itaona namna ya kujipanga, lakini bila kusahau kuwawezesha wanawake kwa kuwasomesha kuwatia moyo, kuwatia nguvu kwamba wanaweza kugombea na kusimama vizuri katika uongozi.
Aidha, Rais Samia alikemea rushwa katika vyama hivyo na kusema kuwa vyama vya siasa vinatakiwa kubadilika kwani mapambano ya rushwa ni ya watu pia uongozi unapatikana bila kutoa rushwa kama ilivyo desturi ya wengi kwenye Vyama vya Siasa.
“Eneo la Rushwa, Sasa hapa ni kidonda ndugu, hakuna hata chama kimoja kilichonusurika na hili, Rushwa siyo zile kubwa lakini hata kama unawalisha wajumbe ili wakupe kura ni Rushwa na hakuna chama ambacho hakifanyi, hii ni tabia ambayo tunatakiwa kubadilisha watu wajue kwamba kuchaguliwa si mimi ni chama leo hii tunashuhudia kwenye vyama vyetu humo Kuna watu hata kusema hawawezi lakini kwa sababu ya rushwa waliweza kupata uongozi”, alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema kuwa Serikali imepokea ripoti hiyo na mambo kadhaa itayafanyia kazi baada ya kujipanga kwa vikosi kadhaa kama vile watunga Sheria, watu wa kuangalia mambo ya siasa, wa kuangalia mambo ya katiba na mambo mengine ambayo Kikosi kimeyaanisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Prof. Rwekaza Mukandala alisema kuwa Kikosi hicho kimeanisha masuala mbalimbali muhimu ambayo yanalenga kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja kwenye suala ya kuhubiri demokrasia nchini.
Kikosi kimebainisha masuala mbalimbali ikwemo Mikutano ya Hadhara na ndani ya Vyama vya Siasa, masuala yanayohusu uchaguzi na mifumo ya maridhiano ili kudumisha amani na utulivu, suala la ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa, elimu ya uraia rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama hivyo, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma pamoja na Katiba mpya”, Alisema Prof Mukandala.
Ili kupata mtazamo Mpana kuhusu masuala 9 yanayofanyiwa kazi, Aprili 14, 2022 Kikosi kazi kilitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kuwaalika Watanzania wote kuwasilisha maoni na mapendekezo kuhusu masuala hayo tisa kwa njia mbalimbali ikiwemo WhatsApp, barua pepe, anuani ya posta ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na pia kuzungumza na wajumbe wa kikosi kazi ana kwa ana.