Serikali imesema inakusudia kukuza utalii wa fukwe, mikutano pamoja na utalii wa kuvinjali kwa meli ikiwa ni mkakati wa kuongeza mazao mapya ya utalii nchini kwa ushirikiano baina ya Tanzania bara na visiwani.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo - S!TE, 2023 jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali itaendelea na jitihada za kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira wezeshi ya kufikia lengo hilo.
Amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwa kinara namba moja wa kukuza sekta ya utalii nchini.
Aidha, amesema Serikali inatambua wajibu huo na imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uwepo wa mazingira yatakayopelekea- utalii endelevu (sustainable Tourism).
“Ni kwa sababu hiyo Ripoti ya Baraza la Utalii na Masuala ya Safari Duniani (World Travel and Tourism Council, WTTC) ya Mwezi Mei, 2022, imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 Bora Duniani kwa uhimilivu wa maeneo yake kupokea watalii (sustainability). Matunda ya hatua zinazochukuliwa na Serikali yanaonekana wazi. Leo hii pamoja na athari za UVIKO19, tunafurahi kwamba, kasi ya kukua kwa sekta ya utalii wetu ni nzuri,” amefafanua Mhe. Kairuki
Waziri Kairuki ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepelekea, Sekta ya utalii kuchangia asilimia 25 ya fedha za kigeni, na asilimia 17.5 ya pato la taifa ambapo amesisitiza kuwa huo ni mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu.
Amesema sekta ya utalii inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wananchi na kwamba Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba sekta hii inabaki kuwa imara, na inazidi kukua.
Pia amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu kama vile barabara, reli na viwanja vya ndege ili kuhakikisha wageni wanayafikia maeneo yote yenye vivutio vya utalii kwa urahisi.
Amesema Serikali imeendelea kuliimarisha zaidi Shirika la Taifa la Ndege la “Air Tanzania” (ATCL) ili kuimarisha usafiri wa anga ambapo amesema katika siku za hivi karibuni ATCL limeanza safari za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda India, China na nchi za jirani ambapo mwakani linatarajia kuanza safari zake barani Ulaya.
Amesisitiza kwamba, kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa, mashirika mbalimbali ya kimataifa yaliyokuwa yamesitisha safari zao wakati wa kipindi cha UVIKO19 yamerejesha safari zao za kuja nchini na mashirika mengine kama Air France, Saudi Airlines, yameanza safari mpya za kuja Tanzania, pia mashirika megine mengi yameanzisha safari maalum “Charted Flights” kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Simai Said kutoka Zanzibar amesema Serikali yake itashirikiana kikamilifu katika kuimbarisha utalii hususan utalii wa fukwe ambapo pia ameshauri kuboreshwa kwa tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mzava amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha utalii nchini na ameshauri kufufua mazao mapya ya utalii, kufungua maeneo maeneo ya kusini na kuunganisha utalii wa Tanzania bara na visiwani.
Maonesho ya S!TE ya mwaka huu yamehusisha waoneshaji zaidi ya 150 na wanunuzi
wa kimataifa wapatao 100 wanaotoka nchi mbali mbali duniani.