Na Mwandishi Wetu, Nairobi-Kenya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Rais mpya wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa karibu zaidi na nchi hiyo ili kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi hizo.
Rais Samia ameeleza dhamira hiyo ya Tanzania leo Septemba 13, 2022 Jijini Nairobi nchini Kenya wakati akitoa hotuba fupi katika Sherehe za kumuapisha Rais wa nchi hiyo, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto.
“Nitumie fursa hii kuihakikishia Kenya dhamira yetu ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuleta maendeleo ya pamoja ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zetu lakini na Ukanda wote wa Afrika Mashariki”, ameeleza Rais Samia.
Mbali na kuihakikishia Kenya ushirik5iano, Mhe. Samia amewapongeza Wakenya kwa kuonesha demokrasia ya hali ya juu na kumaliza uchaguzi salama na kwamba amani waliyoionesha katika uchaguzi ni zawadi kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Fauka ya hayo, Rais Samia amewapongeza Rais Ruto na Makamu wake Mhe. Rigathi Gachagua kwa kuchaguliwa kuiongoza Kenya kwa kipindi cha miaka mitano na pia kumshukuru Rais Mtastaafu Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta kwa kumaliza kuitumikia Kenya kwa mafanikio makubwa.