Na Redempta Ndubuja
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezindua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo mkoani Kagera na kuzindua Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko mnamo 2016.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema Chuo cha VETA kimejengwa kwa shilingi bilioni 22 huku shule ya sekondari ya Ihungo ikijengwa kwa shilingi bilioni 10.9.
“Kuna kero ya kutokamilika kwa jengo la mama na mtoto katika Zahanati ya Buhembe ambapo shilingi milioni 229 zilitolewa na UNDP kwa ajili yaujenzi wa jengo hilo lakini jengo halijakamilika na fedha zimeisha, Mkurugenzi jipange vizuri ili jengo likamilike” amesema Mheshimiwa Rais.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema Chuo cha VETA kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 1,000 wa kozi fupi huku shule iliyojengwa ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,150.
“Pamoja na mradi huu, Serikali inaendelea na ukarabati wa shule kongwe 89 ambapo shule 86 zimeshakarabatiwa na nyingine zipo kwenye za mwisho za ukarabati” amesema Mheshimiwa Waziri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Kaguti amesifu maendeleo yaliyopatikana kwenye sekta ya elimu katika muhula wa kwanza wa utumishi wa Rais Magufuli.
“Ufaulu nao umeongezeka, kwa sasa ufaulu kwenye Mkoa wa Kagera ni asilimia 88.8 kwa shule za msingi na ufaulu wa shule za sekondari umefikia asilimia 90” amesema Mheshimiwa Kaguti.